Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu
Akizungumza na mtandao huu jana kwenye mazoezi ya Simba yanayoendea katika uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam, Kocha Msaidizi Jamhuri Kihwelu, alisema ni lazima wacheze mechi za kupima nguvu kwa sababu timu yao inajengwa upya.
Kihwelu alisema hawajajua watacheza mechi hizo na timu zipi, lakini kwa mujibu wa programu ya mazoezi ya kocha mkuu Abdallah Kibadeni ni lazima wapate mechi mbili kabla ya kwenda Sudan ambako Simba imepangwa kundi A na itafungua dimba na wenyeji El Merreikh.
"Kama unavyoona kikosi ndiyo kwanza kinaanza kupikwa upya, hivyo ili kujua tuna wachezaji wa aina gani tutacheza mechi mbili za kujipima nguvu kabla ya kwenda Sudan," alisema.
Kuhusu kikosi kinachoendelea kujifua Kinesi, Julio alisema wamejitokeza wachezaji mbalimbali zaidi ya 30 wakiwamo wageni kutoka Nigeria, DR Congo na Mzimbabwe ambaye alianza kujifua jana anayeitwa Tinashi Matenence.
"Tunao wanigeria hapa kama wawili, Isdore Modebe na Samuel Okey, Wakongo na Mzimbabwe, Tinash Matenence, japo ukweli nafasi iliyosaliwa kwa mapro ni moja tu ya kiungo kwani nafasi nyingine zimeshapata watu wa kuzicheza," alisema.
Baadhi ya wachezaji wapya wa Simba waliokuwepo mazoezini jana ni pamoja na Ibrahim Twaha 'Messi' na Issa Rashid 'Baba wa Ubaya'.