Katibu
Mkuu wa klabu ya Yanga, Lawrance Mwalusako, amesema klabu yake imefunga
mjadala wa uhamisho wa mchezaji Mrisho Ngasa na sasa inasubiri maamuzi
ya shirikisho la soka, TFF.
Akizungumza jijini Dar es Salaam,
Mwalusako alisema kuwa Yanga haitishiki na madai ya uongozi wa Simba
kuwa mchezaji huyo bado ni wao kwa kuwa Yanga imemsajili Ngassa kwa njia
sahihi na haina shaka ya kutomtumia msimu ujao.
“Yanga ina viongozi makini na tunafanya
kazi kisasa, hili suala la Ngassa kwetu tayari tumelifunga na
tunasubiri kuanza kumtumia kwenye michezo mbalimbali," alisema Mwalusako
na kueleza zaidi, "haya maneno mengine ni ya mkosaji tu. Hutuyaogopi.”
Kauli ya Mwalusako inafuatia kiongozi
mmoja wa Simba kudai wiki hii hawatamruhusu Ngassa kuchezea Yanga bila
kulipwa sh. milioni 25 kama fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wanaodai
kuingia naye; ambao ungeanza kufanya kazi mara baada ya mkopo wake
kumalizika.
Lakini Mwalusako alisema Yanga ilikuwa na
uhakika mchezaji huyo hajasaini timu yoyote kwa ajili ya msimu ujao bali
alikuwa Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja wa mkopo akitokea Azam.
Mchezaji huyo alimaliza mkataba huo mwishoni mwa msimu wa ligi kuu hivyo Yanga ilikuwa sahihi kumsajili, alisema Mwalusako.
“Hayo maneno mengine yanayosemwa nje sisi hatuna la kuongea, sisi tunafuata kanuni za usajili zinasemaje.
"Kamati husika ya usajili ya TFF itaamua na kutoa maamuzi lakini hatuoni cha kuamuliwa kwa sababu kila kitu kipo sawa.”
Mwalusako allisema mchezaji huyo ataanza
kuitumikia Yanga mwezi ujao kwenye mashindano ya Kombe la Kagame la
klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati nchini Sudan.