Mwenyekiti wa Shirikisho la Wasanii nchini, Addo
Novemba aliliambia gazeti hili jana kuwa wanaendelea kuwasiliana na watu
walioko Afrika Kusini ili kujua ni lini utaletwa.
Awali, mwili wa Ngweair aliyefariki Afrika Kusini
alikokwenda kwa shughuli za muziki, ulitarajiwa kuletwa jana, lakini
ilishindikana kufuatia Watanzania wanaoishi nchini humo nao kutaka
kupata fursa ya kuuaga kabla ya kusafirishwa leo.
Novemba alisema ratiba ya awali ilionyesha kuwa
shughuli ya kuuaga mwili wa Mangwea ingeanza saa mbili asubuhi mpaka saa
sita mchana Jumatatu, kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa
mazishi.
Wakati huohuo, Wizara ya Habari, Utamaduni na
Michezo imetoa pole kwa wasanii na wadau mbalimbali wa tasnia ya muziki
kufuatia kifo cha msanii huyo.
“Kifo cha Albert Mangwea ni pigo kubwa kwa fani ya
muziki hapa nchini, na pia kimataifa, ni kutokana na umahiri wake
katika fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya hususan aina yake ya uimbaji
ya “Free Style” alikonga mioyo ya wapenzi wake hasa vijana ndani na nje
ya nchi.” ilisema taarifa hiyo ya Wizara iliyosainiwa na Waziri Fenella
Mukangara.
“Mangwea atakumbukwa na wadau wa muziki kwa kipaji
na juhudi zake za kukuza muziki hapa nchini.Serikali inawapa pole ndugu
na jamaa.”