Upo
uwezekano mkubwa uwanja wa kisasa wa klabu ya Yanga ukajengwa mahali
tofauti na Kaunda kutokana na udogo wa eneo la Jangwani, imeelezwa.
Akizungumza jana, mmoja wa
wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake
kutajwa gazetini kwa sababu si msemaji wa masuala ya uwanja alisema:
Kwa kuangalia michoro ya uwanja mpya na
mahali ambapo klabu inakusudia kujenga uwanja huo, ni vigumu uwanja
ukawa kwenye eneo la Kaunda.
Alisema kutokana na kuwapo kwa ugumu huo,
uongozi unaendelea kuangalia cha kufanya ili kufanikisha ujenzi huo,
ambao umekuwa ukiahidiwa na awamu mbalimbali za utawala wa Yanga kwa
miaka 20 sasa.
Mahasimu wa Yanga kwenye ligi kuu ya Bara,
Simba, wanadai kuwa katika mchakato wa kujenga uwanja wake wa kisasa
katika kitongoji cha Bunju, km 40 kutoka klabuni Msimbazi.
Uwanja wa Kaunda ulijengwa na waasisi wa
klabu hiyo mwanzoni mwa miaka ya 1970 lakini kwa sasa umezungukwa na
makazi ya watu licha ya kuwa kwenye bonde la mto Msimbazi.
Ingawa uongozi wa Yanga ulikaririwa na
gazeti moja mapema wiki hii ukidai umetuma maombi ya kunyakua nyumba
hizo Wizara ya Ardhi, jambo hilo haliwezekani.
Kisheria mikono ya serikali imefungwa
katika kutwaa makazi binafsi hayo kwa sababu uwanja huo si kwa ajili ya
maslahi ya umma hivyo Yanga inatakiwa kushawishi majirani zake hao kuuza
maeneo yao hayo kwake.
"Ukitazama michoro ni wazi pale hapatoshi
lakini bado tunatafutwa njia nyingine za kuona ujenzi huo
unafanikiwaje," alisema mjumbe huyo.
Alipoulizwa kama wanaweza kutafuta eneo
lingine kwa ajili ya ujenzi huo, mjumbe huyo alisema hana uhakika lakini
ikibidi watafanya hivyo.
"Nafikiri ukimtafuta makamu mwenyekiti (Clement Sanga) anaweza akakufafanulia kwa undani zaidi... mimi si msemaji.
"Lakini kikubwa ni klabu kuwa na uwanja
wake hivyo kama pale patashindikana nafikiri kutakuwa na busara ya
kutafuta eneo lingine."
Simu ya mkononi ya Sanga haikuwa ikipatikana alipotafutwa jana, hata hivyo.
Yanga imekabidhiwa michoro ya uwanja wenye
kuketisha watazamaji 30,000 inaokusudia kujenga na mkandarasi kampuni
ya Beijing Construction ambayo moja ya kazi zake nchini ni Uwanja wa
Taifa wenye kuingiza watazamani chini kidogo ya 60,000.