
Rais Jakaya KIkwete akisalimiana na Rais wa Marekani, Barack Obama
katika Ikulu ya White House nchini Marekani. Akiwa nchini Rais Obama
atafanya mazungumzo na Kikwete kisha watafanya mazungumzo ya pamoja na
waandishi wa habari.
Ukitaka kumfahamu mtu, tazama aina ya watu wanaomzunguka. Msemo huu unaweza kutumika kuielezea Tanzania hasa baada ya kupata fursa ya kutembelewa na marais watatu wa taifa lenye nguvu zaidi duniani, Marekani.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilitembelewa na Rais
wa Marekani aliyeko madarakani, George W Bush mwanzoni mwa 2008 na sasa
nchi imepata fursa tena ya kutembelewa na rais mwingine wa nchi hiyo,
Barack Obama ambaye atakuwa ameambatana tena na Bush, jambo ambalo ni la
kihistoria katika Bara la Afrika.
Pamoja na kwamba kuna hali ya kutoridhika na hali
halisi ya nchi, kiuchumi, kisiasa na kijamii kutoka kwa baadhi ya
Watanzania, hali inaonekana kuwa ni tofauti kabisa kwa Marekani ambayo
mtazamo wake wa masuala ya nchi za nje unawakilisha mtazamo wa mataifa
mengi ya magharibi.
Akizungumzia sababu za ziara hiyo kwa njia ya
conference call kutoka Washington, Naibu Mshauri wa Masuala ya Ulinzi wa
Ikulu ya Marekani, Gayle Smith alisema Obama anazuru Tanzania kwa
sababu nchi hiyo ni rafiki mkuu wa Marekani katika Afrika Mashariki na
kwamba imebobea katika misingi ya kidemokrasia.
Smith alisema Bara la Afrika hususan Tanzania ni
moja ya masoko muhimu sana yanayoibukia ulimwenguni na Marekani ni
lazima iongeze harakati zake barani humo.
“Kuna fursa nyingi za kiuchumi, biashara na
uwekezaji jambo ambalo linaitisha umuhimu wa kampuni na biashara za
Marekani kujikita zaidi Afrika,” anasema Smith.
Tofauti na ziara ya Bush ambayo ililenga zaidi
kuisaidia Tanzania kutoa huduma bora kwa watu wake hususan afya; ziara
ya Obama imetokana na maombi na msukumo kutoka kwa wafanyabiashara wa
Marekani ambao waliitaka Serikali yao kuunda mikakati ya makusudi ya
kuhakikisha nchi hiyo inakuza na kuboresha uhusiano wa kibiashara na
Waafrika.
Wakati wa ziara ya George W Bush, Tanzania
ilinufaika na msaada wa dola 698 milioni kwa ajili ya ununuzi wa
vyandarua na dawa za kuulia mbu pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya
Ukimwi.
Maambukizi ya Ukimwi yalianza kushuka mwaka 2008 kutoka asilimia saba mwaka 2003 hadi kufikia asilimia tano na mwaka huu.
Idadi ya watu ambao wanajitokeza kupimwa Ukimwi na
kuchukua majibu yao imeongezeka kutoka asilimia 20 ya wanawake mwaka
2008 hadi kufikia asilimia 30 mwaka 2012 na kwa wanaume imepanda kutoka
asilimia 19 mwaka huohuo na kufikia asilimia 27 mwaka 2012.
Kwa upande wa malaria, kaya tisa kati ya 10
zinatumia vyandarua vyenye dawa ongezeko ambalo ni mara nne zaidi ya
idadi ya kaya zilizotumia vyandarua hivyo mwaka 2004.
Hali kadhalika, zaidi ya asilimia 70 ya watoto
ambao wako hatarini kuambukizwa malaria walilala ndani ya vyandarua
ongezeko ambalo pia ni mara nne zaidi ya idadi ya mwaka 2004.