BONDIA Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’, anatarajiwa kupanda ulingoni kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala, Zakhem, Dar es Salaam, kuzipiga na bondia kutoka Zambia, Darius Lupupa, siku ya Idd Mosi.
Siku hiyohiyo, msanii mkali wa Bongo Fleva ambaye ni adimu sana, Ali Kiba (Pichani), ataongoza timu ya wakali wengine wa muziki, kufanya shoo itakayoacha simulizi.
Meneja Matukio wa Dar Live, Abdallah Mrisho, alisema kuwa pambano la Miyeyusho na Lupupa ni maalum kwa ajili ya kuwapa mashabiki wa ndondi nchini ladha ya kimataifa.
“Julai 7, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Miyeyusho alimchapa vibaya sana bondia kutoka Kenya, Shadrack Muchanje kwa knock out, sasa tunamkutanisha na Mzambia ambaye ni mkali sana,” alisema Mrisho na kuongeza:
“Sasa tutaona kama Miyeyusho ataendeleza rekodi yake au atawaangusha Watanzania. Kila kitu tutakiona Dar Live siku ya Idd Mosi. Siku hiyohiyo, mabondia wenye uzani wa juu, Chupaki Chipindi kutoka Iringa na Ramadhan Kido wa Dar es Salaam nao watakong’otana.
“Kutakuwa na mapambano ya utangulizi vilevile bila kusahau moja la wanawake ambalo litawakutanisha wanawake wenye msuli. Kuhusu burudani, Ali Kiba, Hamisi Ramadhan Baba ‘H. Baba’, TMK Wanaume Family na Mapacha Watatu, watatoa burudani inayokubalika.”
Mrisho aliongeza kwamba kiingilio ni shilingi 10,000 kwa wakubwa na watoto watalipa shilingi 2,000, pia watapata fursa ya kucheza michezo yao yote ambapo siku hiyo, mtaalamu wa kuwaburudisha watoto, Profesa Calabash atakuwepo.