come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

ASHA BARAKA ASHITUKIA MPANGO WA KUTIMKA WANENGUAJI WAKE TWANGA

MKURUGENZI wa African Stars Entertainment (ASET), inayomiliki bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka, amevunja safu ya wanenguaji wa bendi yake kwa kile alichodai utovu wa nidhamu.


Asha, juzi akitumia simu ya kiganjani, aliwaita wanenguaji wote wa kike katika ofisi za ASET, zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam, akiwaeleza kuwa kuna kikao.

Alipofika katika ofisi hizo, Asha alikwenda katika kikao hicho ambacho pia Kiongozi wa bendi, Luiza Mbutu, alikuwapo, na kubainisha kuwa amesikitishwa na tabia ya wanenguaji hao kutangaza kwenda katika Falme za Kiarabu kunengua bila ya kufuata taratibu za kiofisi, ikiwa ni pamoja na kuacha mshahara wa mwezi mmoja.

“Mimi nimechoka na utovu wenu wa nidhamu, mnaondoka bila kuaga halafu pindi mnapomaliza mikataba yenu huko Dubai mnarudi kimyakimya hapa, hii bendi ya kwenu?” alihoji Asha.

Alisema kwa sasa anaivunja hiyo safu ya wanenguaji wote na kuanzia leo yule ambaye anajiona anahitaji kubaki Twanga atalazimika kujisajili upya na kuacha namba zake za pasi ya kusafiria ambazo atazipeleka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

“Mnanichezea sana na sasa nawatangazia rasmi kuwa nitakuwa na roho mbaya, yale mambo ya kuleana hapa sasa hayapo tena, kwangu mnatoroka kazini halafu mkirudi mmekondeana, hamna lolote mnalolipata huko Dubai, bora ‘m-make’ hapa hapa Bongo mnakookota shilingi mbili, tatu, ushamba tu wa kupanda ndege ndio unawasumbua,” alisika Asha akifoka na kuongeza:

“Eti mnanitishia, hii bendi mmeikuta, walikuwapo wanenguaji wa kutisha kama Aisha Madinda, Lilian Internet, hamnitishi, mimi nasema nendeni salama tu wala sijali,” alisema Asha kwa ukali.

Tanzania Daima ilipomuuliza kwa nini ameivunja safu hiyo, Asha alibainisha kuwa wanenguaji hao walikuwa wamepanga kutimkia Falme za Kiarabu kwa kazi hiyo hiyo ya kunengua, lakini alipozipata tetesi hizo ndipo alipoamua kuwatema wote kabla wao hawajafanya hivyo.

Aidha, alijinadi kwamba hababaishwi, kwani tayari ameshatangaza nafasi za wanenguaji wapya. Wanenguaji ambao hawakutaka kujisajili tena ni pamoja na Mary Kimwana, Baby Tall na Sabrina Pazi.