come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KIINGILIO CHA KUZIONA SIMBA NA URA HIKI HAPA

WAKATI kikosi cha timu ya soka ya URA ya Uganda kikitarajiwa kuwasili nchini leo tayari kuivaa klabu ya Simba Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam keshokutwa, viingilio katika mchezo huo vimetajwa ambapo cha chini ni sh 5,000.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa ziara ya URA, George Wakuganda (Pichani) , alisema wameamua kuweka viingilio vya hali ya kawaida ili kutoa fursa kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo.

Alisema kiingilio hicho kitahusisha watakaokaa viti vya kijani, bluu na orange huku VIP B ni sh 15,000 na VIP A ni sh 20,000.

Wakuganda aliongeza kuwa maandalizi kwa ajili michezo hiyo yanakwenda vema na lengo la mechi hiyo ni kukipima kikosi cha Simba, pia sehemu ya utambulisho wa wachezaji wapya watakaoitumikia katika msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Agosti mwaka huu.

Naye Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kikosi cha Simba kilichokuwa kwenye ziara maalumu ya kimichezo katika mikoa ya Tabora, Katavi na Mara kinatarajiwa kurejea jijini leo.

Wakati huo huo, katika kuelekea mkutano mkuu wa Simba Jumamosi, wanachama wa Tawi la Mpira Pesa, wamewataka wanachama wengine wa klabu hiyo kujitahidi kadiri wawezavyo kuhudhuria kwa wingi ili kuushughulikia ipasavyo uongozi wao, ambao unaonekana kutofuata katiba.

Kauli ya tawi hilo, imetoka siku moja baada ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, kutangaza kuwafuta uanachama wale ambao watazungumza na vyombo vya habari juu ya mkutano huo uliopangwa kufanyika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Akizungumza na Tanzania Diama jana, Mwenyekiti wa tawi hilo, Ustadh Masoud, aliwaomba wanachama kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo ambao umesigina katiba, ili muafaka ukapatikane siku hiyo, kwa kuwa uongozi umekwenda kinyume cha katiba kwa kutangaza siku 14 kabla badala ya siku 30 kama katiba yao Ibara ya 20 (1 na 2), kinavyowataka.

Ustadh pia alimtaka Rage kuhakikisha anawaonyesha kipengele ambacho kinampa uwezo kuwafuta uanachama wale watakaozungumza na vyombo vya habari na endapo atafanikiwa, watampa zawadi ya sh milioni moja kwa ajili ya futari katika mfungo huu wa Ramadhani, kwani atakuwa amewasaidia wengi kujua katiba na kuacha kuzungumza na vyombo vya habari.

“Tunawahimiza sana wanachama wenzetu wa Simba kuja siku hiyo na kulipia kadi zao ili tuje tuushughulikie vema uongozi, ambao unakwenda kinyume cha katiba ya klabu, tunataka kujua kipengele kinachotuzuia kusema madukuduku yetu kwa wanahabari, halafu yeye anasema akisikia mtu anamfukuza, aseme ni kipengele gani?” alihoji Ustadh.