Ernest Brandts
Akizungumza jana jijini, Brandts alisema kutokuwepo kwa wachezaji walio katika kambi ya Taifa Stars kunafanya kazi yake ya maandalizi ya msimu ujao kuwa ngumu.
"Mimi kama kocha nina programu zangu ambazo ningependa nizitoe kwa wachezaji wangu wote lakini unaona? Kuna wengine hawapo na sisi, wapo kwenye timu ya taifa," alisema Brandts.
"Sasa inanipa ugumu kwa sababu nataka kutengeneza timu ambayo itafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa."
Alisema ingawa ligi kuu ya Bara imepangwa kuanza mwezi ujao, maandalizi anayofanya ni kwa kuzingatia zaidi michezo ya kimataifa, hususani Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Kwa kurefusha rekodi na kutwaa ubingwa wa 23 wa ligi kuu ya Bara msimu uliopita, Yanga itacheza Ligi ya Klabu Bingwa ya Afrika inayoanza miezi saba ijayo.
"Kwa sasa siandai timu kwa ajili ya ligi kuu peke yake," alisema Brandts, kwa sababu "sisi ndio wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
"Hivyo lazima tujiandae vizuri."
Stars imeweka kambi kwa ajili ya hatua ya mtoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, dhidi ya Uganda ambapo mchezo wa kwanza utakuwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.
Akizungumzia kikosi chake alisema kwa sasa anaona kimekamilika kwa kuwa wachezaji aliokuwa akiwataka amewapata.
"Tangu nilipokuja hapa niliwaambia viongozi wamsajili Ngasa (Mrisho), kwa sababu ni mchezaji mzuri na atatupa msaada mkubwa na pia Mustapha (Ali) alikuwa anaitaji msaidizi mwenye uwezo mkubwa na tumefanikiwa kumpata Dida (Deogratius Munishi).
"Kwa sasa ni kujiandaa tu na mashindano ya mbele yetu," alisema Brandts.
Yanga kesho inacheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Kampala City Council kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kabla ya kurudiana na wageni hao katika miji ya Shinyanga na Tabora.