Suala
la ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Yanga sasa limerudishwa kwenye ngazi
ya majadiliano mapya na uongozi wa klabu hiyo, imeelezwa.
Akizungumza na mtandao huu Makamu
Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema ujenzi wa uwanja mpya
umeshindwa kuanza mwezi uliopita kama walivyokuwa wamepanga lakini
wanaendelea kutafuta suluhisho la jambo hilo.
Awali Yanga ilikuwa ianze ujenzi wake
mwezi uliopita baada ya kupokea michoro kutoka kwa kampuni ya Beijing
Engineering Construction ya China, lakini ikadaiwa kuwa umeshindikana
baada ya eneo la Uwanja wa Kaunda kuwa dogo kulinganisha na michoro.
Sanga, alisema kamati ya utendaji itakutana ili kuangalia njia ya kufanya ili kufanikisha ujenzi wa uwanja huo wa kisasa.
"Bado kama klabu tupo kwenye mchakato wa ujenzi wa uwanja wetu," alisema Sanga na kueleza zaidi:
"Lakini kama nilivyosema awali, eneo limeonekana kuwa dogo hivyo kamati itakutana kuangalia upya nini cha kufanya."
Alisema kamati ya utendaji itakutana wakati wowote kuanzia kesho Jumatatu kujadili jambo hilo.
Hata hivyo Sanga hakutaka kuelezea kama
klabu itakuwa tayari kutafuta eneo lingine kwa ajili ya ujenzi huo, kama
ambavyo kiongozi mmoja aliiambia NIPASHE mwishoni mwa wiki iliyopita.
"Kila kitu kikikamilika tutawaeleza, kwa
sasa inakuwa ngumu kuzungumzia hatma yake kwa sababu bado hatujakutana
kujadili jambo hilo," alisema na kusisitiza, "ngoja tusubiri tukutane."