come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

CHANETA YAWAANGUKIA WADAU

MWENYEKITI wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Annie Kibira (Pichani) , ametoa wito kwa wapenzi na wadau wa michezo nchini kutangaza bidhaa na huduma zao kupitia mchezo huo kwa lengo la kuusaidia kupiga hatua zaidi kwa maslahi ya vijana na taifa.


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kibira alisema ili mchezo wa netiboli upige hatua, wadau mbalimbali wanaombwa kujitokeza kuudhamini.

“Kiukweli jukumu la kuendeleza mchezo huu sio la sisi tuliopo madarakani, ni jukumu la wadau wote na wananchi kwa ujumla, hivyo tunaomba wadau wajitokeze kutusapoti kwa njia mbalimbali,” alisema Kibira.

Kibira aliwasihi wanafunzi kujitokeza kushiriki mchezo huo katika ngazi mbalimbali kama mashindano ya Shule za Msingi (Umitashumta), na Sekondari (Umisseta), akisema hiyo ni fursa ya kuonekana kwa ajili ya kuteuliwa kwenye timu ya taifa ‘Taifa Queens’.

“Vijana wengi huwa wanatokea katika shule za msingi na sekondari, kwa kufanya hivi tutakuwa na wachezaji wazuri ambao wanaliwakilisha taifa, maana kijana mdogo anapopewa mafunzo ni tofauti na mtu mzima,” alisema.