come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KASEJA YAMKUTA MENGINE.........

Kukwama kwa kipa Hussein Sharrif 'Casillas' kujiunga na FC Lupopo baada ya klabu yake ya Mtibwa kushindwa kuafikiana bei ya kumuuza na timu hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumemkosesha nafasi kipa Juma Kaseja (Pichani) aliyenyimwa mkataba mpya wa kuendelea kuidakia klabu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba.


Kaseja ambaye ni nahodha na pia kipa chaguo la kwanza la timu ya taifa (Taifa Stars), alitajwa mara kadhaa kuwa yuko mbioni kujiunga na Mtibwa ili aanze kuidakia katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa klabu hiyo ya Manungu, Turiani Morogoro, Jamal Bayser,  aliuambia mtandao huu jana kuwa mpango wao wa kumsajili Kaseja umefutwa baada ya Casillas kutouzwa kwa Lupopo kama walivyotarajia.

“Baada ya Sharrif kubaki, sasa hatuna nafasi ya kusajili kipa mwingine,” alisema Bayser.

Katika hatua nyingine, Bayser alisema vilevile kwamba klabu yao haina mpango wowote wa kusajili mchezaji kutoka nje ya nchi na badala yake wataendelea kuwaamini vijana wazawa kama walivyofanya msimu uliopita na kumaliza ligi wakiwa katika nafasi ya tano.

Kwa wiki moja sasa kulikuwa na tetesi kwamba Kaseja aliyemaliza mkataba wa kuichezea Simba angetua Mtibwa Sugar au Coastal Union ya Tanga.

Hata hivyo, Coastal nayo ilishakanusha taarifa za kutaka kumsajili kipa huyo aliyeidakia Simba kwa takriban muongo mmoja.