KITUO kikubwa cha soka cha kulea vijana wadogo ‘Soccer Academy’ kinatarajiwa kuanzishwa na mdau wa michezo kutoka nchini Ufaransa, Damian Sellier (Pichani), katika eneo la Liganga mji mdogo wa Usa River wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Akizungumza mjini hapa jana, Sellier alisema amelazimika kuanzisha kituo hicho baada ya kuvutiwa na wananchi wa eneo hilo kupenda michezo hususan soka, lakini wakikosa uwezo wa kuwandaa vijana wao kuwa wachezaji bora.
“Nilifika hapa na kuamua kushirikiana na kituo cha Usa River Youth kuanzisha mashindano maalumu ya vijana chini ya miaka 15 na chini ya miaka 20, ambapo watu wengi wamejitokeza kuyaunga mkono na hivyo kunifanya nishawishike kuanzisha kituo hicho cha vijana,” alisema Damian.
Alifafanua kuwa mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo Agosti na yanayoshirikisha timu 14, ataondoka kwenda Ufaransa kwa ajili ya kuweka mambo sawa tayari kuanzisha kituo hicho atakaporejea akiwa na vifaa kamili.
Naye mratibu wa Usar river Youth, Daudi Mkumba, akizungumzia mpango huo alisema wao kama kituo kilichosajiliwa, waliamua kushirikiana na mdau huyo kusimamia mashindano aliyoyaanzisha kwa kuwa anapenda michezo.
“Huyu bwana anapenda mpira; akawa anataka kuanzisha mashindano ya vijana kwa kuwa hajawa na taasisi yoyote iliyosajiliwa hapa nchini, akaamua kuja kutushirikisha sisi ili tusimamie michezo hii kupitia taasisi yetu na tunaendelea naye vizuri,” alisema Mkumba.
Alifafanua kuwa tayari Mfaransa huyo ana taasisi yake aliyoanza kuisajili iitwayo Help Development Sports For Tanzania Children, ambayo ndiyo itakuwa inamiliki kituo hicho anachotaka kuanzisha, ambapo pia ana mpango wa kujenga uwanja wa kisasa.
