MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, wamesema kwamba aliyekuwa kiungo wake mshambuaji, Hamis Kiiza, anajua kila kitu kinachoendelea kuhusiana na suala la kuongezwa mkataba mpya.
Hatua hiyo inakuja kutokana na nyota huyo raia wa Uganda, kudaiwa kuwa na mvutano na uongozi wa klabu hiyo juu ya kusaini mkataba mpya, kwa madai anataka kulipwa dau la dola 50,000 za Marekani badala ya 35,000 ambazo Yanga iliweka mezani.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, kiongozi mmoja wa Yanga alisema kwamba wameamua kuachana kwanza na suala la Kiiza, kutokana na nafasi yake kutokuwa na umuhimu katika kikosi hicho.
Kiongozi huyo alisema wameshamueleza Kiiza kuwa kwa sasa hana nafasi, kwani Yanga inahitaji mshambuliaji halisi mmoja, ambaye atashirikiana na aliyepo sasa, Mrundi Didier Kavumbagu.
“Kwa sasa suala la Kiiza tumeliweka kando, kwani nafasi yake haina umuhimu katika kikosi chetu, tunatafuta mshambuliaji halisi, ila tukikosa ndipo tutarudi kwake,” alisema.
Akienda mbali zaidi, kiongozi huyo alisema kwamba mshambuliaji huyo anafahamu kila kitu juu ya mustakabali wake ndani ya klabu hiyo na hata hilo suala la kumpa fedha anayoitaka yeye halipo.
Aliongeza kuwa baada ya kumleta mshambuliaji kutoka Nigeria, Ogbu Brendan, kwa ajili ya majaribio, hivi karibuni tena wataleta washambuliaji wengine kujaribiwa.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kimeendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara, ambapo keshokutwa itacheza mechi ya kirafiki na URA ya Uganda.
