Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage jana alitoka nje ya Ukumbi wa
Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oyesterbay chini ya ulinzi mkali baada ya
kumalizika kwa mkutano wa klabu hiyo, ambao wanachama walishindwa
kujadili kwa kina ajenda kutokana na vurugu na zomeazoea.
Kabla hata ya kufanyika mkutano huo, tayari
kulikuwa na makundi ya wanachama wakiupinga na ndiyo hao ambao walitumia
fursa ya kushiriki kwao kwenye mkutano kumzomea Mwenyekiti Aden Rage.
Mwenyekiti Rage alijikuta kwenye wakati mgumu
kutokana na baadhi ya wanachama kumzomea wakati akiwasomea maelezo ya
mikakati na maendeleo ya klabu hiyo, ingawa mwishoni alifanikiwa
kuwatuliza baadhi ya waliompinga.
Kasheshe ya kuzomea-zomea iliendelea hata baada ya
kuitwa mbele Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Tolly Mbwete kuzindua mpango
mkakati wa maendeleo ya klabu hiyo.
Wakati Mbwete (Profesa) akisoma maelezo ya mkakati
huo, baadhi ya mashabiki walisikika wakisema;
“Hatutaki...hatutaki...toka, hatutaki kusikia habari ya Chuo Kikuu,
tunataka matokeo mazuri uwanjani huo mkakati wenu hautusaidii.”
Pamoja na kuzomewa, Rage alimtaka Mbwete kuendelea
kusoma maelezo ya mkakati huo huku kelele zikiongezeka kutoka kwa
wanachama wengi, hali iliyowafanya wengine kushindwa kusikiliza
kilichokuwa kikiongelewa.
Kama mwendelezo wa kupinga kilichokuwa
kikiongelewa, baadhi ya wanachama waliondoka kwenye mkutano huo uliokuwa
chini ya ulinzi wa askari zaidi ya 70.
Baada ya mambo kwenda vibaya, Rage aliwataka
polisi kuwakamata wanachama waliokuwa wakifanya fujo ikiwa ni pamoja na
kuwatishia kuwafuta uwanachama, jambo lililoibua zogo zaidi.
“Hatoki mtu hapa...tupo tayari kufa lakini hapa
hatoki mtu...unatuburuza, hatukutaki...tumekuchoka ondoka,” wanachama
walipaza sauti.
Mkutano huo, uliofunguliwa saa 3 asubuhi na
kuhudhuriwa na wanachama 712 kati ya 1516 ambao ni hai, na wanachama hao
walishindwa kuchangia kikamilifu ajenda hali iliyopelekea mambo mengi
kupitishwa kienyeji.
Kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Simba
ilipata kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa
dhidi ya timu ya URA kutoka Uganda.
Simba walikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika
ya saba likifungwa na Betram Mombeki. URA walisawazisha kupitia kwa
Lutimba Yayo dakika 60, na kisha akafunga bao la ushindi dakika ya 76.