TIMU ya taifa ya soka Tanzania, ‘Taifa Stars’ imeendelea kujifua jijini Mwanza kujiwinda na mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo dhidi ya Uganda ‘The Cranes’.
Mchezo wa marejeano kusaka nafasi ya kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Nyota Wanaocheza Ligi za Ndani, utapigwa dimba la Mandela huko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala, huku Stars ikiwa na kibarua kizito, baada ya kukubali kulala kwa bao 1-0 nyumbani Jumapili iliyopita.
Akizungumza kwa simu kutoka jijini Mwanza jana, Meneja wa timu hiyo, Leopold Tasso Mukebezi, alisema kuwa kila Mtanzania na benchi la ufundi wamesikitishwa na kiwango kilichoonyeshwa katika mchezo wa awali.
Aidha, Mukebezi alisema kwa sasa Kocha, Kim Poulsen, anajitahidi kuangalia sehemu zenye upungufu ili aweze kuzifanyia kazi kabla ya marudiano, kwa kuwa Stars bado ina uwezo wa kuwafunga Uganda nyumbani kwao, kwani mpira ni dakika 90.
“Ninajua matokeo haya yamemsononesha kila mtu, hata sisi benchi la ufundi tumesikitika sana, lakini imetokea na Kim na msaidizi wake wanaangalia wapi kuna makosa ili aweze kuyarekebisha kabla ya mchezo wa marudiano,” alisema Mukebezi.
Alisema Stars kwa sasa inafanya mazoezi mara moja kwa siku kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ambako imeweka kambi katika Hoteli ya Lacairo.
Stars ili iweze kufuzu inatakiwa ishinde 2-0.
