Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb alisema mwishoni mwa wiki kwamba, kocha wao, Ernie Brandts alipendekeza kambi katika ya mwisho kuelekea mechi hiyo na Azam.
Hata hivyo, Kleb hakusema kambi itakuwa wapi, zaidi ya kusema itakuwa hapa hapa nchini- ingawa tunafahamu kipaumbele ni Pemba na kama si huko itakuwa Bagamoyo.
Kwa sababu hiyo, Yanga SC inaweza kuingia kambini mwishoni mwa wiki hii, kwani Jumamosi ya wiki ijayo ndiyo siku ya mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tayari kikosi cha mabingwa hao wa Bara kimekwishakamilika baada ya wachezaji wake wote waliokuwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars akiwemo Mrisho Ngassa kuanza mazoezi.
Yanga SC ndiyo timu pekee kati ya zile tano bora kwa sasa katika Ligi Kuu, ambayo haijangia kambini.
Coastal Union wapo kambini Raskazone Hotel, Mtibwa Sugar wapo kambini Dar es Salaam, Simba SC wapo kambini Bamba Beach, Kigamboni na Azam FC wapo Afrika Kusini.
Azam jana ilianza vibaya ziara yake ya mechi za kujipima nguvu Johannesburg, baada ya kufungwa mabao 3-0 na wenyeji, Kaizer Chiefs katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa mazoezi wa wa timu hiyo, eneo la Nachurena.
Azam ambayo imefikia katika hoteli Towers eneo kla Randburg, katika mchezo huo iliathiriwa na uchofu wa safari na hali ya hewa ya baridi, hivyo kucheza chini ya kiwango na kupewa kipigo hicho.
Azam leo inatarajiwa kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Wits University asubuhi na jioni na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall amefurahishwa na mazingira ya kambi na Uwanja wa mazoezi.
Baada ya mazoezi ya leo, Azam itashuka tena dimbani kesho kumenyana na Mamelodi Sundowns kabla ya kuivaa Orlando Pirates Agosti 9 na Agosti 12 itamaliza ziara yake kwa kumenyana na Moroka Swallows.
Azam inatarajiwa kurejea nchini Agosti 13 tayari kwa mchezo wa kuwania Ngao dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.