Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kurudisha rufaa ya Yanga iliyopinga adhabu ya mshambuliaji wao Mrisho Ngassa (Pichani) kufungiwa mechi sita na faini ya 45 milioni, uongozi wa Yanga umepanga kulipeleka suala hilo Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Hivi karibuni uongozi wa Yanga uliwasilisha rufani yao kupinga adhabu ya Ngassa aliyopewa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF baada ya kamati hiyo kubaini kuwa mshambuliaji huyo alisaini mkataba mkataba wa mwaka mmoja Simba kabla ya kutua Yanga.
TFF walirudisha barua ya rufani ya Yanga kwa madai kuwa haitambui barua hiyo imeelekezwa kwa kamati gani ya rufaa ya TFF kwa sababu kuna kamati ya rufaa ya ligi inayoongozwa na Jaji Benard Luanda na kamati ya maadili ya uchaguzi inayoongozwa na Steven Ihema.
Hata hivyo kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga kililithibitisha kuwa baada ya TFF kurudisha barua hiyo, uongozi wa Yanga umepanga kupeleka suala hilo CAF baada ya kubaini kuwa hakuna kanuni ambayo inatoa adhabu hiyo.
‘’Sisi tulichokifanya tuliamua kumpa kazi Patrick Nagi ambaye ni mmoja wa viongozi wa kamati ya utendaji ya Yanga kufuatilia suala hilo CAF na wakatujibu hakuna kanuni kama hiyo na hata kwenye barua ya TFF hawajaandika wametumia kanuni gani,’’ alisema mmoja wa viongozi wa kamati ya utendaji ya Yanga.
Mtandao huu ulipoongea na Kaimu Katibu wa Yanga, Lawrance Mwalusako ambaye alisema kuwa hivi sasa hawezi kuongea lolote, lakini wanasubiri viongozi wote warudi Dar es Salaam baada ya mchezo wa jana dhidi ya Prisons uliochezwa Sokoine mkoani Mbeya ndipo watalitolea uamuzi.
Alisema uamuzi utatolewa na kamati ya utendaji ambayo itakutana kwa ajili ya kujadili suala hilo na kuhakikisha wanamsaidia mchezaji huyo kucheza Yanga msimu huu.