Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
inayoongozwa na Jaji Steven Ihema imewarudisha wagombea saba
walioenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na kamati ya uchaguzi
ya TFF iliyo chini ya Hamidu Mbwezeleni.
Kamati hiyo iliyokutana juzi iliamua kuwarejesha wagombea wote kwenye uchaguzi kwa kile kilichoelezwa kuwa hawana hatia.
Wagombea
ambao wamerudishwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni Kilungeja Nazarius,
Riziki Juma, Wilfred Kidau, Shaffih Dauda, Omary Abdukadir na Richard
Rukambura.
Rukambura anayewania nafasi ya rais alienguliwa kwa
kile kilichoelezwa kuwa alifungua kesi mahakamani kwenye uchaguzi wa
awali uliofutwa akipinga kuenguliwa na Omary Nkwaruro aliyeenguliwa
baada ya cheti chake kuwa na utata.
Dauda alienguliwa kwa kile
kilichoelezwa kumiliki nyaraka za mawasilino za siri kati ya Tenga na
Fifa na kuzisambaza kwenye mtandao wa kijamii, huku Kidau akienguliwa
kwa kutumia nyaraka za kamati ya utendaji bila idhini.
Kwa upande
wa Nazarius alienguliwa kwa madai ya kusababisha migogoro katika Chama
cha Soka cha Rukwa, wakati Riziki Juma aliondolewa kwa kushindwa
kusimamia kanuni za ligi akiwa mtendaji mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa
Pwani (Corefa) kipindi cha ligi ya mkoa na mmoja wa wadau wa soka
akafungua kesi mahakamani.
Abdukadir alienguliwa kwa kushindwa kuheshimu maagizo ya TFF waliposimamisha uchaguzi wa (FRAT).
Wagombea
wote mbali na sababu nyingine walizotoa, pia walijitetea kuwa Fifa
iliagiza mchakato wa awali ufutwe kila kitu na kuanza mchakato mwingine
hivyo hawana hatia.