come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

Uganda yatibua dili ya Kapombe Ulaya



Beki wa Simba na timu ya Taifa ya Tanzania, Shomari Kapombe amehairisha safari yake ya kufanya majaribio na timu ya FC Twente ya Uholanzi ili aweze kuitumikia  Taifa Stars katika mchezo wa CHAN dhidi ya Uganda.

Kapombe ambaye alipaswa kuondoka nchini wiki ijayo, alisema kuwa amekwisha wasiliana na wakala wake kuhusiana na kuharisha kwa zoezi hilo na sasa atakwenda Uholanzi Julai 15 kuanza majaribio.
Alisema kuwa mawazo yake yote kwa sasa ni kwenye mchezo wa CHAN dhidi ya Uganda kwani wana usongo na timu hiyo ili kuweza kusonga mbele katika mashindano hayo.
“Nilitakiwa niondoke wiki ijayo, lakini kutokana na majukumu ya Timu ya Taifa, nimeamua kuahirisha safari hiyo na sasa nataka kulitumikia taifa langu kwanza, nataka kuona tunafika wapi baada ya kukosa nafasi ya kufuzu kwa ajili ya Fainali ya  Kombe la Dunia ya mwakani,” alisema Kapombe.
Alisema kuwa mechi dhidi ya Uganda ni muhimu sana na wanatakiwa kupata ushindi mkubwa hapa nyumbani ili kuweka mazingira mazuri katika mechi ya marudiano.
Alifafanua kuwa safari yake ya huko ipo chini ya wakala mmoja wa kimataifa na mbali ya FC Twente ambayo inacheza Ligi Kuu ya Uholanzi ijulikanayo kwa jina la Eredovisie, pia anatarajia kufanya majaribio katika timu mbalimbali nyingine atakazopangiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zacharia Hanspoppe alithibitisha mabadiliko hayo kwa Kapombe na kusema kuwa wao wanaweka mbele maslahi ya Taifa na kuomba  kusogezwa mbele kwa majaribio hayo.
Hanspoppe alisema kuwa wamekwisha wasiliana na wakala huyo ambaye hakutajwa jina kuhusiana na mabadiliko ya tarehe ya kufanya majaribio na wamekubaliana naye.
“Sisi hatuna vipingamizi kwa Kapombe na mchezaji mwingine yeyote ambaye atataka kwenda nje kufanya majaribio kwa sababu tunajali masilahi yao,  Taifa na klabu kwa ujumla, hatutaki kung’ang’ania mchezaji ambaye timu nyingine zimeonyesha kumpenda.”
Alisema kuwa wao wanajiandaa vyema kwa ajili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara huku wakifanya usajili wao kwa uangalifu mkubwa.