Simba ilitolewa pia katika hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kupokea kipigo cha jumla ya mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo de Libolo ya Angola.
Okwi aliuzwa kwa ada ya dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 480) kwa klabu ya Etoile du Sahel inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia, fedha ambazo zimebaki kuwa hadithi kwani hadi sasa Simba haijalipwa na Waarabu hao.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema kuwa kuondoka kwa Okwi kulichangia kuiyumbisha klabu yao katika mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu uliopita kwani nyota huyo anayetegemewa pia na timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) alikuwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu kikosini mwao.
Rage alisema jambo jingine ambalo Simba halitarudia ni kuuza mchezaji kwa 'mali kauli' kwani wamejifunza kutokana na namna wanavyozungushwa fedha zitokanazo na mauzo ya Okwi; na ambazo kuzikosa kuliifanya klabu yao ishindwe kusajili nyota waliowatarajia msimu huu.
"Tuliathirika sana, tumeyumba na tumeshindwa kusajili wachezaji tuliowataka kutokana na kukosa fedha haraka kama tulivyotarajia. Jambo hili liko wazi, hatutarudia tena kuuza mchezaji kwa mali kauli," alisema Rage.
Alisema kwamba ukongwe na utajiri wa Etoile du Sahel ndiyo uliwafanya waamini kuwa watawalipa fedha hizo mapema, lakini machafuko ya kisiasa yaliyoikumba Tunisia na klabu hiyo kutumikia adhabu ya kucheza mechi bila ya mashabiki ni sababu nyingine zilizochangia Simba kuchelewa kulipwa fedha hizo.
Aliitaja sababu nyingine iliyowafanya Simba wamuuze Okwi huku akiwa na muda mfupi tangu asaini mkataba mpya wa kuichezea Simba ni kutokana na nyota huyo kufanya mazungumzo ya awali na kuwa, kama wangechelewa mshambuliaji huyo angeondoka klabuni hapo mchezaji huru.
Rage pia aliwatoa hofu wale wanaodhani kuwa fedha za Okwi zimeliwa na viongozi kwa kusema hakuna kitu kama hicho na kuahidi kuwa kila kitu kitawekwa wazi pindi watakapolipwa kwani matumizi yake yatakuwa ni kutekeleza mipango ya maendeleo ya klabu hiyo.
"Tuliandikiana mkataba mpya na tayari umesajiliwa Fifa... hivyo malipo yatakapofanyika yataonekana katika mtandao. Siku hizi hauwezi kufanya ubabaishaji kama huko nyuma ilivyokuwa ambapo watu walikuwa wanaweza kujifungia ofisini na kumaliza mazungumzo," aliongeza Rage.
Katika hatua nyingine, Rage alisema kwamba wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba walitarajiwa kukutana jana jioni kupanga mikakati mbalimbali ya msimu ujao na maandalizi ya mkutano mkuu wa klabu hiyo ambao huenda sasa ukafanyika Agosti 4 jijini Dar es Salaam.
Rage pia alikanusha taarifa za kufanya mazungumzo na aliyekuwa kipa chaguo la kwanza la timu hiyo, Juma Kaseja, kama ilivyotangazwa jana mchana na kituo kimoja cha redio.
'Suala la Kaseja tumeshalifunga," alisema Rage kumzungumzia Kaseja ambaye bado ni kipa chaguo la kwanza na nahodha wa timu ya taifa (Taifa Stars).