WACHEZAJI wa Azam FC wameshutumiwa kwa kucheza pasipo kujituma uwanjani, hali ambayo imesababisha timu hiyo kutoa sare tatu katika mechi nne za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Azam jana ililazimishwa sare ya 1-1 na timu dhaifu, Ashanti United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wake wa nne wa Ligi Kuu na wa kwanza nyumbani msimu huu.
Awali, katika mchezo wa kwanza ililazimishwa pia sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro kabla ya kutoa sare kama hiyo na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, ikitoka kushinda 2-0 dhidi ya Rhino Rangres Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.
Habari za ndani kutoka Azam zinasema kwamba viongozi na Wakurugenzi wa timu, wanalia na wachezaji kutojituma licha ya kupewa maslahi mazuri na maandalizi mazuri.
Ikumbukwe, kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, Azam iliweka kambi ya wiki mbili Afrika Kusini ikijifua na kucheza mechi za kirafiki dhidi ya timu bora za huko, lakini tangu imerejea nchini imashinda mechi moja tu na Rhino.
Ilifungwa na Yanga 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii kabla ya sare tatu na Mtibwa, Kagera na Ashanti. Sare dhidi ya Ashanti ndiyo imeuumiza zaidi uongozi na baadhi ya Wakurugenzi, kwa kuwa wanaamini hiyo timu dhaifu.
Azam sasa inajiandaa kwa mchezo wake wa tano wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga SC Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo, zinafungana kwa pointi sita kila moja baada ya mechi nne za awali. Ikumbukwe Yanga ni mabingwa watetezi na Azam ni washindi wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita.