come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA YANUSURIKA KIPIGO MORO, IVO AFUNGWA GOLI LA KIZEMBE.

SIMBA SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar iliyomaliza pungufu ya mchezaji mmoja baada ya Nahodha wake, Shaaban Nditi kuonyeshwa kadi nyekundu kipindi cha pili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Hadi mapumziko tayari Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi dakika ya nane.

Akapiga mpira unaofanana na krosi ambao ulielekea kwenye himaya ya kipa Ivo Mapunda, lakini kwa bahati mbaya mpira ukamteleza kipa huyo na pamoja na jitihada za kutaka kuurejesha mikononi mwake, ukadondokea  nyavuni.
 
Simba SC ilipigana kuanzia dakika ya tisa kutaka kusawazisha bao hilo, lakini hawakufanikiwa hadi zilipotimia dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic alimtoa nje kiungo Awadh Juma Issa dakika ya 36 akamuingiza mshambuliaji Ali Badu Ali na kidogo safu ya ushambuliaji ilichangamka.


Kipindi cha pili Simba SC ilicharuka na kufanya mashambulizi ya nguvu lango ni mwa Mtibwa, hatimaye kupata bao la kusawazisha dakika ya 50, mfungaji Mrundi Amisi Tambwe, aliyemalizia pasi ya Haroun Chanongo.
 
Mtibwa ikapata pigo dakika ya 69, baada ya Nahodha wake, Nditi kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumtolea lugha chafu refa Deonisia Kyura wa Arusha.

Matokeo hayo yanaifanya Simba SC itimize pointi 31 baada ya kucheza mechi 16 na kupanda hadi nafasi ya tatu mbele ya Mbeya City yenye pointi 31 pia, lakini Wekundu wa Msimbazi wana wastani mzuri zaidi wa mabao, 18 kwa 9 ya Mbeya City. Yanga SC ni ya pili kwa pointi zake 35 na Azam FC yenye pointi 36 inaongoza ligi hiyo, wakati Mtibwa Sugar inatimiza pointi 22 baada ya kucheza mechi 16 pia hivyo kubaki nafasi ya tano.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Haruna Shamte/Said Ndemla dk65, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Donald Mosoti, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhan Singano ‘Messi’, Amri Kiemba, AMisi Tambwe, Awadh Juma/Ali Badru na Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk51.

Mtibwa Sugar; Hussein Sharrif ‘Casillas’, Hassan Ramadhani, Said Mkopi, Salim Abdallah, Salvatory Ntebe, Shaaban Nditi, Ally Shomary/Juma Mpakala dk73, Juma Luizio/Vincent Barnabas dk66 Mussa Hassan Mgosi/Abdallah Juma dk87 na Jamal Mnyate.