Shamra shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Miraji Kikwete na Aima Mahmoud wakiondoka kwenye ukumbi wa Mlimani City baada ya kufunga ndoa yao jana
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni waalikwa. Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo ndani na nje ya ukumbi huo.
Miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Wengine waliokuwepo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Inspekta Jenerali Omari Mahita, Mkurugenzi wa Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Issa Shaaban Simba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadicky.