Rais Wa Marekani Barrack Obama amekiagiza kitengo cha ujasusi nchini humo kusitisha ukusanyaji wa habari kutoka kwa simu za mamilioni ya raia nchini humo na hata katika mataifa ya kigeni.
Akizungumza mjini Washington Obama pia amewaahidi viongozi wa nchi washirika wa Marekani kwamba taifa lake halitachunguza mawasiliano yao ya faragha hadi itakapolazimika kufanya hivyo kutokana na maswala ya ki-usalama.
Tangazo hilo linajiri wakati ambapo kuna hasira ya kimataifa kuhusiana na kiwango cha upelelezi unaofanywa na Marekani kufuatia ufichuzi wa siri za kitengo hicho uliofanywa na aliyekuwa mchambuzi wa maswala kijasusi nchini humo Edward Snowden.
Mwandishi wa BBC mjini Washington amesema kuwa makundi ya wanaharakati watashangazwa na hatua ya kitengo hicho kuendelea kumiliki habari nyingi za simu walizokusanya na kwamba haijulikana watazifanyia nini habari hizo.
Hadhi ya kitengo cha ujasusi nchini marekani imeshushwa na ufichuzi wa bwana Snowden.
Wakati huohuo hotuba ya rais Obama kuhusu mabadiliko ya mpango wa upelelezi wa marekani yamepongezwa nchini Ujerumani.
Uhusiano kati ya Berlin na Washington uliwekwa katika mizani mwaka uliopita baada ya kubainika kwamba marekani ilidukua simu ya chansela wa Ujerumani Angela Merkel.