KIUNGO wa Ivory Coast,Yaya Toure anaendelea kuimarika kwa kasi kuelekea katika mchezo wa ufunguzi wa kombe la dunia dhidi ya Japan jumamosi, amesema kocha Sabri Lamouchi.
Toure ameshindwa kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake tangu alipofanyiwa upasuaji mwezi uliopita.
Lamouchi amesema timu ya madaktari wa Ivory Coast inajitahidi sana kuhakikisha mchezaji huyo bora wa mwaka wa Afrika anacheza wakati nchi yake itakapoanza mchezo wa ufungizi wa kundi C dhidi ya Japan mjini Recife.
'Tunafanya kila linalowezekana ili acheze" kocha aliwaambia waandishi wa habari.
Toure alipata majeruhi katikati ya mwezi aprili mwaka huu, lakini alirudi uwanjani kuisaidia Manchester City kutwaa ubingwa wa pili katika misimu mitatu.
Halafu akaenda Qatar kwa ajili ya matibabu na baadaye alijiunga na kikosi cha Ivory Coast kwenye kambi ya mazoezi huko America.
Toure hakucheza mechi mbili za kupasha pasha dhidi ya Bosnia na El Salvador.