come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

COUTINHO ASHANGAZWA NA UBORA WA WACHEZAJI YANGA, ADAI ATAPIGANIA NAMBA

Kiungo mpya wa kimataifa wa Yanga kutoka Brazil, Andrey Coutinho, amesema hana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, hivyo atahakikisha anapambana ili kuweza kupata nafasi ya kucheza.


Coutinho aliwasili nchini Ijumaa iliyopita akitokea Brazil na kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga.

Akizungumza katika mazoezi ya jana asubuhi, Coutinho, alisema yeye ni mchezaji mzuri lakini bado anaamini kuna baadhi ya vitu atajifunza kutoka kwa wachezaji wa Yanga na wao pia watajifunza kutoka kwake ili kuifanya timu hiyo iwe na kiwango cha juu.

Coutinho ambaye alikuwa anazungumza kwa lugha ya kwao Brazil (Kireno) na kutafsiriwa na -kocha msaidizi wa timu hiyo, Leonardo Neiva, kwamba haifahamu Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara lakini kupitia mazoezi atajua mbinu za wachezaji wa hapa nchini.

"Nimekuja Yanga kuendeleza kipaji changu, naamini kuna vitu nitajifunza kutoka kwa wachezaji wenzangu na wao watajifunza pia kutoka kwangu," alisema kiungo huyo.

Alisema hatabweteka katika mazoezi licha ya kusajiliwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo huku uongozi ukiwa haumfahamu.

Kiungo huyo alionyesha kuwa mwepesi na akishiriki kikamilifu mazoezi ya ufukweni na kila mara akicheka na wachezaji wenzake wa timu hiyo alikabidhiwa jezi namba saba huku kiungo, Omega Seme, ambaye amerejea Yanga akitokea Prisons alikopelekwa kwa mkopo, naye amekabidhiwa jezi namba 14 ambayo msimu uliopita ilikuwa inavaliwa na beki, Rajab Zahir.

Habari zaidi kutoka Yanga zinaeleza kuwa uongozi wa timu hiyo umemtuma kiongozi Brazil ili kusaka nyota mwingine atakayesajiliwa na timu hiyo.

Mpango huo wa kutafuta mchezaji mwingine wa kimataifa huenda ukaipa nafasi Yanga kusitisha mkataba wake na mshambuliaji kutoka Uganda, Hamisi Kiiza, ambaye naye ameonekana kuwaletea 'pozi' mara kwa mara.

Wachezaji wengine wa kigeni ambao wako Yanga ni pamoja na beki Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima (Rwanda) na Emmanuel Okwi wa Uganda.