come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAXIMO AIPIGISHA TIZI LA NGUVU YANGA

Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo ameanza kazi yake kwa kishindo jana asubuhi na jioni kwa kuwakimbiza wachezaji wake kwa saa mbili kwenye ufukwe wa Coco na Uwanja wa Bandari, jijini Dar es Salaam.


Mbrazili huyo akisaidiwa na wasaidizi wake Leonardo Neiva na Juma Pondamali, ametumia mazoezi hayo kwa lengo la kuwapa nguvu za mwili wachezaji wake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.

Ingawa nyota wengi wa kikosi cha kwanza hawakuwepo katika mazoezi hayo na kufanya wachezaji 13 pekee, lakini idadi ya wachezaji hao iliongezeka kufuatia Mbrazil huyo kujumuishwa na wale wa timu ya vijana ambao walikuja na kocha wao Salvatory Edward aliyekuwa akishiriki kumsaidia Maximo.


Nyota hao wote walifanya mazoezi makali ya mbio ndefu pembezoni mwa Bahari ya Hindi  katika fukwe za Coco kabla ya kugeukia yale ya viungo ambayo yalikuwa yakitolewa na kusimamiwa na Neiva huku Maximo akifuatilia ufanisi wa kila mchezaji akiwa pembeni.

Jeshi kamili la Yanga likivifua kikamilifu chini ya kocha anayeogopwa Marcio Maximo katika fukwe za Coco jijini Dar es Salaam.

Kivutio katika mazoezi hayo alikuwa ni Maximo wakati wachezaji wa kikosi hicho wakikimbia mbio ndefu alijumuika pamoja nao kuanzia mwanzo hadi mwisho wa zoezi hilo jambo ambalo liliwapa shida nyota wavivu kushindwa kutegea mazoezi.

Akizungumza kabla ya mazoezi hayo Maximo alisema anataka kuanza kuimarisha nguvu ya miili kwa nyota wake kwa mazoezi ambayo watakuwa wakiyafanya asubuhi, lakini jioni watageukia yale ya ufundi ambayo yatakuwa yakifanyika uwanjani.

“Natarajia tutakuwa tunajifua mara mbili kwa siku, asubuhi tunaweza kuwa huku ufukweni au sehemu nyingine yoyote. Kikubwa ni kutafuta nguvu ya mwili na pumzi, lakini jioni tutakuwa na sehemu nyingine ya mazoezi kwa kufanya yale ya uwanjani,” alisema Maximo.

Uwanja wa mazoezi wawatoa jasho

Wakati Maximo akitangaza ratiba hiyo, Yanga imeonekana kuhaha kila kona ya jiji la Dar es Salaam kusaka sehemu ya uwanja mzuri wa mazoezi.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini Yanga walitaka kufanya mazoezi katika Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika  huko Oysterbay, lakini ikashindwa kuupata uwanja huo kutokana na wenyeji kuufanyia maboresho.

Mbrazil. huyo Coutinho akijifua vikali na wenzake tayari kwa maandalizi ya klabu bingwa Afrika mashariki na kamti yanayotarajia kuanza huko Rwanda.

“Yanga waliomba kufanya mazoezi hapa, lakini tumeshindwa kuwapa ushirikiano kutokana na sasa uwanja wetu kuwa katika maboresho. Tumeweka mbolea na nyasi ili zikue vizuri wakati huu ambao wanafunzi wetu wapo kwenye mapumziko,” alisema mmoja wa walimu wa shule hiyo.

Wakati hali ikiwa hivyo katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika pia Yanga imesita kwenda kuuomba ule wa Bocco Veteran ambao walikuwa wakiutumia msimu uliopita chini ya kocha Hans Pluijm  kwa sababu ilikuwa ikidai ada kubwa. Klabu hiyo ilikuwa ikitoa kiasi cha sh 350,000/= kwa siku.