come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAXIMO AWASIFU WACHEZAJI YANGA, ADAI WALIPIGANA

Kocha wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo ameelezea kukasirishwa na kipigo dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini amewaambia wachezaji wake kwamba amefurahishwa na namna walivyopigana mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo.

Yanga juzi ilikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Akizungumza na wachezaji wake mara baada ya mechi hiyo Maximo alisema "nataka kila mmoja anisikilize kwa makini, nimekasirika sana kwa kipigo hiki lakini mmenifurahisha kwa namna mlivyopigana mwanzo mwisho".


Hata hivyo, awali Maximo ambaye hiyo ni mechi yake ya kwanza ya ligi, alisema kwamba mechi ijayo anaamini atafanya vizuri na kwamba kiungo wake Mbrazil mwenzake Andrey Coutinho atakuwapo uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.

Alisema kwa ujumla Mtibwa walicheza vizuri katika dakika 15 za mwanzo na kwamba mchezo wa soka ndivyo ulivyo huwezi kushinda siku zote kwani mara nyingine unaweza kushinda na kushindwa.

Maximo alisema kilichobaki sasa ni kujipanga kwa mechi ijayo kwani hakutegemea kukutana na matokeo kama hayo ingawa hawezi kuwalaumu wachezaji wake kwa kuwa walionyesha kujituma kiume mwanzo hadi mwisho.

Kwa upande wa kocha wa Mtibwa Mecky Mexime alijivunia kupata ushindi dhidi ya kocha wake wa zamani lakini akasema huo ni wa Watanzania wote kwa kuwa ameonyesha wazawa wanaweza.Yanga haina rekodi nzuri ya kuifunga Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, kwani mara ya mwisho kuibuka na ushindi dimbani hapo ilikuwa Septemba 19, 2009 iliposhinda mabao 2-1.

Katika mechi nyingine zilizopigwa juzi, mabingwa watetezi Azam FC walianza vema kulitetea taji lao nyumbani kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Polisi Morogoro.

JKT Mgambo ikiwa nyumbani ilishinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar wakati Mbeya City yenyewe ikitoka suluhu na JKT Ruvu huku Ruvu Shooting ikikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Wageni wa ligi hiyo, Ndanda FC wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga walianza kwa kishindo kwa kuwafunga wageni wenzao wa Ligi Kuu, Stand United kwa mabao 4-0 na kukaa kileleni mwa kinyang'anyiro hicho kinachoshirikisha timu 14.