come
PHIRI AIPONDA SIMBA YAKE, ADAI NI MBOVU KILA IDARA
Sare ya pili mfululizo ambayo Simba imepata katika mechi yake ya juzi imemchanganya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri, alisema jana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Phiri, alisema hajafurahishwa na matokeo hayo ya juzi na kwamba timu ilicheza chini ya kiwango ukilinganisha na ilivyocheza katika mechi ya kwanza dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Phiri alisema sehemu ya kiungo bado haijaonyesha kiwango cha juu kama ambavyo amewaandaa katika maandalizi.
Alisema pia bado mfumo wa kutumia washambuliaji wawili, Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe haujazoeleka lakini anaamini katika mechi zinazofuata Simba itaonekana tofauti.
"Sijafurahia matokeo ya sare, bado tunahitaji kupambana ili timu ishinde, tulivyocheza na Coastal Union na mechi ya Polisi, hali ilikuwa tofauti...kiufupi timu haikucheza vizuri," alisema Phiri.
Mzambia huyo alisema kila siku anawakumbusha wachezaji kuwa makini zaidi wanapokuwa wanaongoza, kwa sababu uliyemfunga anabadilika na kujipanga kurekebisha makosa yake na kwamba hapo wao ndipo wanapofungwa na kupoteza muelekeo.
Aliongeza kuwa, Simba bado inachangamoto ya kusaka ushindi na kurejesha heshima yake katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.Alisema ligi ni ngumu na kila timu inaingia uwanjani kusaka pointi tatu.
"Siwezi kuizungumzia Yanga ambayo ilianza kwa kufungwa, ila nasema Ligi Kuu sasa imekua na ushindani mkubwa kuliko miaka ya nyuma nilivyoiacha," Phiri alisema. "Nafahamu mashabiki na wanachama wa Simba wana kiu ya ushindi nitahakikisha nawapa furaha msimu huu."
Simba ilianza kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union na juzi ililazimishwa sare ya 1-1 na Polisi ya mkoani Morogoro.