Kipa chaguo la kwanza wa timu ya Simba, Ivo Mapunda, jana aliungana na kikosi cha timu hiyo jijini Johannesburg, Afrika Kusini huku akishuhudia wakifungwa mabao 4-2 dhidi ya Bidvest Wits University katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Starock Park.
Katika mechi ya kirafiki iliyochezwa jana asubuhi, Simba ilimaliza kipindi cha kwanza ikiwa imelala mabao 2-1.
Kipa chipukizi, Peter Manyika 'Junior' ndiye alikuwa langoni dakika zote 90 kutokana na Hussein Shariff 'Casillas' kuwa majeruhi wakati wafungaji wa mabao ya Simba jana walikuwa ni Ramadhani Singano 'Messi' na Elias Maguri.
Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kikosi cha Simba sasa kiko kamili huko Johannesburg baada ya Mapunda na wachezaji wengine watano wa timu hiyo ambao walikuwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars) iliyokuwa na mechi ya kirafiki juzi dhidi ya Benin, nao kuwasili salama Afrika Kusini jana asubuhi.
Aveva aliwataja wachezaji hao ambao walishuhudia timu yao ikilala kuwa ni pamoja na Amri Kiemba, Haroun Chanongo, Said Ndemla, Elius Maguri na Jonas Mkude.
Alisema kikosi cha timu yao sasa kimekamilika na kwa sababu wachezaji waliobaki nchini ambao walikuwa kwenye timu ya Taifa, wataendelea na mazoezi na hawatakuwa nyuma.
Aliongeza kuwa, baada ya Casillas kuvunjika mguu katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Jumamosi dhidi ya Orlando Pirates, leo uongozi ulilazimika kumuongeza Mapunda kwenye kambi hiyo baada ya kumuacha kwenye kundi la kwanza ambalo liliondoka nchini Jumatano iliyopita kutokana naye kuuguza jeraha la kidole.
Kikosi cha Simba leo kinatarajia kushuka dimbani kucheza mechi ya tatu ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Jomo Cosmos ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo. Pia Simba kesho Jumatano itacheza mechi nyingine.