Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Mfungaji wa bao la kusawazisha la Mtibwa Sugar, Mussa Hassan 'Mgosi' amesema amefurahi kuwa yeye ndiye mfungaji wa bao katika mechi dhidi ya Simba ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1 na kuwafunga 'mdomo' waliokuwa wanamkejeli.
Mgosi ambaye aliwahi kuzichezea Simba na JKT Ruvu, alifunga bao hilo katika dakika ya 58 na kuwanyamazisha Simba ambao walitangulia kufunga katika dakika ya 34 ya mchezo huo kupitia kwa nahodha wao, Joseph Owino.
Akizungumza mjini hapa, Mgosi, alisema yeye ni mchezaji wa Mtibwa Sugar, hivyo juzi uwanjani alikuwa akijituma na kutekeleza maelekezo ambayo timu hiyo ilipewa na benchi la ufundi.
Mgosi alisema wadau wa soka wanatakiwa kuachana na dhana potofu ya kuamini mchezaji ambaye ameihama timu atashindwa kuonyesha kiwango chake wakati atakapokuwa anacheza dhidi ya timu yake ya zamani.
"Mimi si Simba, niliwahi kuichezea Simba, mimi kwa sasa ni Mtibwa Sugar, nitaifanyia kazi Mtibwa Sugar, naomba ieleweke hivyo," alisema Mgosi.
Alisema kwamba ligi ni ngumu tofauti na miaka ya nyuma hivyo kila timu inasaka matokeo mazuri hasa katika mzunguko wa kwanza wa ligi.
"Tunataka kushinda, tunacheza kwa bidii muda wote, hakuna ambaye hapendi ushindi, hata Simba pia ilijiandaa kushinda, mechi imeisha inabidi sote tukubaliane na matokeo, ila nimefurahi kuona bao la Mtibwa nimefunga mimi," Mgosi aliongeza.
Alisema hadi sasa bado hakuna timu yenye uhakika wa kutwaa ubingwa msimu huu kutokana na matokeo yanayopatikana katika mechi zinazoendelea kuwashangaza wadau wa soka nchini.
"Unapotarajia kushinda hali inakuwa tofauti, hakuna mteremko, kikubwa ni kucheza mpira ili kupata ushindi, siku hizi hakuna timu kibonde," alisema Mgosi.
Mgosi alitua Simba mwaka 2005 akitokea Mtibwa Sugar akisajiliwa sambamba na Nico Nyagawa na amewahi pia kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
