Wakati kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm ameeleza kupewa somo na kikosi cha Azam FC katika mechi yao ya juzi, wapinzani wao wamesema waliathiri na ukubwa wa mechi katika mipango yao ya kupata ushindi.
Yanga ilikuwa mwenyeji wa Azam FC katika mechi kali ya raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliyomalizika kwa sare ya mabao mawili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Mara tu baada ya mechi hiyo Pluijm aliyerejea nchini kuifundisha tena Yanga, alisema Azam FC imeonesha upungufu uliopo katika kikosi chake huku akiahidi kuufanyia kazi kabla ya kuwavaa Mbeya City katika mechi yao ya Januari 3 mjini Mbeya.
Alisema Yanga ilikuwa na kila sababu ya kupata ushindi katika mechi hiyo ya kwanza kwake tangu akabidhiwe timu akirithi mikoba ya Mbrazil Marcio Maximo aliyetimuliwa lakini iliponzwa na makosa waliyofanywa na mabeki wa viungo.
"Kulikuwa na tatizo la kukosa mawasiliano baina ya mabeki wetu, viungo pia waliwaacha mno Azam watawale mchezo hasa kipindi cha kwanza. Azam wametuonesha udhaifu wetu, tuna kazi ya kuurekebisha kabla ya kuendelea na mechi zinazofuata.
"Siku zote huwa nasema soka ni mchezo wa makosa, hili ndilo lililotokea leo (juzi), unapocheza dhidi ya timu kubwa kama Azam halafu unakosa mnakosa mawasiliano, lazima utafungwa. Sitaki kumlaumu mchezaji mmoja mmoja maana ukiangalia si (Deogratius Munishi) Dida peke yake alifanya makosa, safu nzima ya ulinzi haikuwa sawa" alisema zaidi kocha huyo.
Kwa upande wake kocha mkuu wa Azam FC, Mcameroon Joseph Omog, ukubwa wa mechi hiyo uliwafanya nyota wake wacheze kwa presha kubwa.
Alisema kikosi chake kilicheza vizuri lakini kiliathiriwa na presha ya kila timu kutaka kushinda mechi hiyo ili kuipuka Mtibwa Sugar kileleni mwa msimamo.
"Tumeshindwa kupata pointi tatu dhidi ya Yanga, tunapaswa kuyasahau matokeo hayo ili tujipange kwa mechi inayofuata dhidi ya Mtibwa Sugar," alisema Omog.
Yanga na Azam ziko nafasi za pili na tatu katika msimamo wa VPL zikiwa na pointi 14, mbili nyuma ya vinara Mtibwa Sugar baada ya timu zote kucheza mechi nane.