MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga Mrundi Amissi Tambwe ameanza kuwarudhia makombora viongozi wa Simba pamoja na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mzambia Patrick Phiri ambao walisema hana kiwango na wakaamua kumtema.
Tambwe alianza kuwajibu viongozi wa Simba pamoja na mashabiki wao kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara kati ya timu yake mpya Yanga SC na Azam FC uliofanyika uwanja wa Taifa jijini.
Katika mchezo huo timu hizo mbili zenye uhasimu mkubwa kwa sasa zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2, Tambwe alikuwa wa kwanza kwa upande wa Yanga kufunga bao zuri la kichwa kufuatia pasi nzuri iliyopigwa na kiungo Salum Telela, goli hilo lilikuwa la kusawazisha baada ya Didier Kavumbagu kutangulia kufunga kwa upande wa Azam.
Tambwe alisajiliwa na Simba msimu uliopita baada ya kuvutiwa naye akiwa na kikosi cha Vital'0 ya Burundi, Tambwe aliichezea timu hiyo ya Burundi ambayo mwaka jana ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la Kagame huku yeye akiibuka mfungaji bora.
Baada ya hapo alisajiliwa na Simba SC na kuanza kuitumikia kwenye ligi kuu bara, alicheza kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu bara kwa kufikisha magoli 19, aliweza kufunga hat trick tatu zaidi huku moja akifunga magoli manne dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga ambapo Simba ilishinda mabao 6-0.
Simba ilibadili makocha watu mfululizo ambapo Tambwe wawili aliweza kuendana nao, alianza na mzalendo Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio', makocha hao waliiwezesha Simba kumaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya tatu.
Walifutwa kazi na kuajiliwa Mcrotia Zdravko Logarusic ambaye alianza kazi kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga, katika mchezo huo Yanga ilifungwa mabao 3-1 huku Amissi Tambwe akiwa mwiba mchungu kwa Yanga baada ya kufunga magoli mawili.
Licha ya kufunga mabao hayo Tambwe aliendeleza moto wake kwenye ligi kuu bara, alifanikiwa kuinusuru timu hiyo isifungwe kwenye mechi zake za ugenini ambapo mara kadhaa amekuwa akiisawazishia Simba.
Tambwe na wenzake waliiwezesha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne ya msimamo wa ligi, Logarusic anaye akatupiwa virago na safari hii Simba ikaamua kumrejesha kocha wake wa zamani Mzambia Patrick Phiri.
Ujio wa Phiri haukuwa na maana tena kwa upande wa Tambwe, hapo ndio ukawa mwisho wake kwani Phiri hakutaka kumtumia hata kidogo, Licha ya kutomtumia Tambwe lakini Simba haikuweza kuchomoza na ushindi zaidi iliweza kluambulia sare sita mfululizo huku ikishinda kamchezo kamoja tena kwa mbinde dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani.
Ushindi huo ulisherehekewa na mashabiki wa Simba na waliamini hawataweza kupoteza tena, Tambwe badpo aliendelea kusota benchi, lakini mwanzoni mwa ligi hiyo wakati Simba ilipocheza na Coastal Union na kutoka sare ya 2-2 Tambwe alifunga bao zuri la kichwa.
Hapa Tambwe akishangilia moja ya mabao aliyofunga msimu uliopita akiwa Simba SC
Wapo walioamini kuwa Tambwe amekwisha, na wapo walioamini kuwa Tambwe anabaniwa tu na kocha au kuna kiongozi fulani haeleweni naye na ndio maana anapata mtihani huo, dirisha dogo la usajili lilifunguliwa novemba 15 na kufungwa desemba 15 ambapo Simba ilitumia nafasi hiyo kusajili nyota wengine wapya na kuachana na wale wa zamani.
Hapo ndipo Amissi Tambwe alipofunguliwa mlango wa kutoka, yeye na ndugu yake Pierre Kwizera waliachwa na kuwapisha Waganda Simon Sserunkuma na Juuko Murushid, Tambwe alisajiliwana Yanga na muda mfupi alianza mazoezi yaliyokuwa chini yake Mbrazil Marcio Maximo ambaye naye akatupiwa virago na kumpisha Mholanzi Hans Van der Pluijm na msaidizi wake Charles Boniface Mkwassa.
Mambo yameenda vema, Tambwe alianza kazi yake kama sehemu ya kuwajibu maadui zake Simba, katika mchezo wake wa kwanza Tambwe alifunga bao zuri mno baada ya kuunganisha mpira wa Salum Telela, goli hilo alilifunga dhidi ya Azam FC ambapo walitoka sare na Yanga 2-2.
Tambwe ameendeleza makali yake kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea huko Zanzibar, ameweza kupika mabao mawili ambayo kama si juhudi zake sidhani kama Yanga ingeweza kuchomoza na ushindi.
Viongozi wa Simba pamoja na wanachama wake kusikia Tambwe ameanza kung'ara akiwa na Yanga tayari wamemtupia virago kocha wao Patrick Phiri kwa madai kwanini amemtema Tambwe wakati ni bonge la straika, Tambwe ni zaidi ya washambuliaji wapya wa Simba iliowasjili hivi karibuni baada ya kumtema Tambwe.
Washambuliaji wapya waliosajiliwa na Simba ni Dan Sserunkuma na kaka yake Simon Sserunkuma, Dan alikuwa anaichezea Gor Mahia ya Kenya na alikuwa mfungaji bora misimu miwili mfululizo wakati Simon alikuwa Express ya Uganda.
Lakini cha kushangaza washambuliaji hao hawajafunga hata bao moja kwenye mechi za mashindano, Dan amecheza mechi tano wakati Simon amecheza mechi tatu, ila Tambwe amefunga bao moja na kutengeneza mawili kwenye mechi za mashindano zinazotambuliwa na TFF.
Amissi Tambwe akidhibitiwa na wachezaji watatu wa Azam FC lakini alifanikiwa kuwatoka
Amissi Tambwe amezaliwa miaka 26 iliyopita jijini Bujumbura na anacheza nafasi ya sentafowadi ana uzito wa kilo 70, alianza kuichezea Vital'0 tangia mwaka 2010 na kudumu nayo hadi 2013 na mwaka 2014 alisajiliwa na Simba ambayo amedumu nayo msimu mmoja na sasa ni mchezaji wa Yanga.
Tambwe atakuwa tegemeo kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Yanga hasa katika michuano ya kombe la Shirikisho, akizungumza hivi karibuni alisema kwanza amefurahi kujiunga na Yanga kwakuwa aatapata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa tofauti na Simba ambao hawana nafasi hiyo.
Vile vile Tambwe amesema ana hasira na timu yake ya zamani Simba hasa kwa kitendo chake cha kumtupia virago, anadai amedhalilishwa mno na Simba na ikiwa yeye ni mchezaji wa kimataifa, anawashukuru Yanga kwa kutambua umuhimu wake na amepanga kuipa zawadi kubwa kutoka mguuni kwake, Tambwe amedai lazima aitungue Simba akikutana nayo.