RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kwamba siku hizi watu wanapenda umaarufu wa vyeo vya klabu na vyama vya michezo, lakini si kufanya kazi
ndiyo maana michezo inadumaa nchini.
Akizungumza katika hafla maalum ya kuagwa na wanamicheo, iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ukumbi wa Mlimani, City, Dar es Salaam,
Rais Kikwete alisema anashangaa kwa nini michezo nchi hii haiendelei.
Rais Kikwete alisema haoni sababu ya michezo kutoendelea nchini wakati kuna mazingira mazuri na katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake alijitolea mno kusaidia michezo.
Alisema kubwa alilofanya ni kusaidia wataalamu kwa kuhakikisha kila mchezo unapata kocha naye ndiye anawalipa mishahara, lakini ajabu baadhi ya vyama vya michezo vilishindwa kundelea kufanya hivyo.
“Netiboli walianza vizuri, walikwenda hadi Singapore kwenye mashindano ya dunia, lakini baadaye kilichowatokea sijui
nini nini,”alisema.
Rais Dk. Jakaya akasema vyama vinaweza hata kuajiri makocha wazawa na wakaendelea kulipwa kama walivyokuwa wanalipwa makocha wa kigeni.
Akawageukia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao
wameamua
kuachana na makocha wa kigeni na kuajiri mzalendo, Charles Boniface Mkwasa akiwaambia kwamba wahakikishe wanamlipa kama walivyokuwa wanalipa Wazungu.
Rais Kikwete amesema kwamba msaada wake wa mwisho ambao anawaachia wanamichezo wa Tanzania, ni kituo cha kulea
vipaji vya wanamichezo wadogo cha Symbion Power kilichopo eneo la
Amesema kituo hicho kilichojengwa kwa msaada wa klabu ya Sunderland ya England kina vifaa na viwanja vya michezo aina yote, ukiwemo wa mpira wa kikapu wa kiwango cha viwanja vya
Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA).
Pamoja na hayo, Rais Kikwete aliwashukuru TASWA kwa kumuandalia shughuli hiyo na akasema atamshauri mgombea
Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli aendelee kuikumbatia michezo.
Katika sherehe hizo za jana, Rais Kikwete alikabidhiwa tuzo
na TASWA kumshukuru kwa mchango wake mkubwa michezoni kwa
kipindi cha miaka 10 ya utawala wake.
Aidha, naye Rais huyo kipenzi cha Watanzania alikabidhi tuzo kwa Wanamichezo 10 waliofanya vizuri wakati wa utawala wake. Rais pia alikabidhi tuzo kwa viongozi mbalimbali waliofanya
vizuri pamoja na wafanyabiashara na asasi zilizomuunga mkono katika kupiga jeki maendeelo ya michezo nchini.
Wanamichezo waliopata tuzo ni Wanariadha Samson Ramadhan aliyepata Medali ya Dhahabu mwaka 2006 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, Martin Sule aliyepata Medali ya Fedha
katika Michezo ya Afrika mwaka 2007 na Mary Naali aliyepata Medali ya Shaba mwaka 2008.
Kikosi cha Taifa Stars kilichocheza CHAN ya kwanza mwaka
2009 kilipata tuzo, mchezaji Nitiboli Mwanaidi Hassan, bondia Francis Cheka, kocha Charles Boniface Mkwasa kwa kuiwezesha
timu ya wanawake, Twiga Stars kucheza fainali za Afrika na mshambuliaji Mbwana Samatta kwa mafanikio yake TP Mazembe wote walipokea tuzo.
Upande wa viongozi Jenerali Mstafu Waitara kwa kujenga
Uwanja wa Gofu, Kanali Mstaafu Iddi Kipingu kwa uwekezaji wake katika michezo ya vijana, Dioniz Malinzi kwa kujenga Uwanja
wa Gofu Bukoba, Leodegar Tenga kwa kuifanya TFF kuwa taasisi yenye kuheshimika na Mtangazaji Abdallah Majura kwa kuweza kuanzisha kituo chake mwenyewe cha Redio (ABM).
Makampuni na wadau waliopewa tuzo ni pamoja na Bakhresa Limited kwa mchango wao mkubwa michezoni na TSN pia.
Rais Kikwete aliyeiongoza nchi tangu mwaka 2005, anamaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu na anatarajiwa kukabidhi
madaraka baada ya uchaguzi Mkuu mapema mwezi ujao