come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

Hanspope akataliwa kujiuzulu Simba

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga.

Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amekataliwa kujiuzulu, imefahamika.
Badala yake, Hans Poppe ambaye aliandika barua ya kujiuzulu hivi karibuni kutokana na mwenendo mbaya wa timu yao na kutaka wanachama wengine wapate nafasi ya kuleta mafanikio, ameundiwa timu maalum ya kwenda kumshawishi ili abadili uamuzi kwani mchango wake unahitajia sana kwa maendeleo ya 'Wanamsimbazi'.

Akizungumza jana, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa kikao cha kamati ya utendaji ya klabu yao kilichofanyika jijini Dar es Salaam juzi jioni na kuongozwa na mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, kimekataa ombi la Hans Poppe na kuridhia ombi jingine la kujiuzulu kwa aliyekuwa makamau mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu'.

Akieleza zaidi, Kamwaga alisema kuwa kwa kauli moja, kikao cha kamati ya utendaji kimeamua kuwa mwenyekiti (Rage) ashirikiane na wadau wengine kwenda kuzungumza na Hanspoppe na kumshawishi abadili uamuzi wa kujizulu kwani hata wanachama wengine wa Simba

waliokutana katika matawi mbalimbali wameeleza kwamba nguvu ya kiongozi huyo (Hanspoppe) bado inahitajika  kwa maendeleo ya timu yao.

"Kuhusiana na Kaburu, kamati imeridhia kujiuzulu kwake na kumshukuru kwa mchango alioutoa ndani ya klabu... na wajumbe wanaamini kwamba ataendelea kuwa sehemu ya Simba," aliongeza Kamwaga.

Kaburu pia aliwasilisha barua ya kuachia ngazi saa chache tu baada ya Hanspoppe kuchukua uamuzi huo, huku naye akisema kuwa anafanya hivyo ili kutoa nafasi kwa wanachama wengine kuongoza kwa imani kuwa wataipa mafanikio zaidi timu yao.
Hanspoppe hakupatikana jana kuelezea msimamo wake baada ya kamati ya utendaji kumkatalia kujiuzulu.

MKUTANO MKUU
Katika hatua nyingine, kikao cha kamati ya utendaji Simba kimeamua vilevile kuwa mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo ufanyike Julai.

Kamwaga alisema kuwa mkutano huo utafanyika kwa mujibu wa katiba yao ambayo inaelekeza kuwapo kwa mkutano mmoja ndani ya mwaka na kwamba, taratibu zaidi kuhusiana na maandalizi ya mkutano huo zitatolewa baadaye.

"Kamati ya utendaji ambayo iliongozwa na mwenyekiti wetu (Rage) iliamua kupanga mkutano huo kwa kufuata maelekezo na ushauri waliopokea kutoka TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)," alisema Kamwaga, huku akiwataka Wanasimba kuwa watulivu na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kamati hiyo pia iliiachia kamati yao ya ufundi na benchi la ufundi kuamua hatma ya wachezaji saba wa timu hiyo ambao wameonekana kutokuwa na nidhamu katika vipindi tofauti msimu huu.

Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Haruna Moshi 'Boban', Amir Maftah, Juma Nyosso, Ramadhan Chombo 'Redondo', Mwinyi Kazimoto, Paul Ngalema na Komabil Keita.

Kamwaga aliongeza kuwa suala la wachezaji Felix Sunzu na Abdallah Juma, ambao tayari walishaandika barua ya kujieleza kutokana na tuhuma za utoro, liko mikononi mwa kocha Patrick Liewig ambaye naye alitarajiwa kutangaza uamuzi wake jana jioni; kama ni kuwaruhusu wajiunge na wenzao na kuendelea na mazoezi au kuwazuia.

Taarifa ya mkutano mkuu wa Simba kutakiwa usubiri hadi Julai huenda ikaibua manung'uniko kutoka kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ambao kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa wakitaka wakutane mapema ili kujadili mwenendo wa kusuasua wa timu yao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na pia kutolewa kwao mapema katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kufuatia kipigo cha jumla ya mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo de Libolo ya Angola.

Hivi karibuni, baadhi ya wanachama wa mabingwa hao wa ligi kuu ya Tanzania Bara walikutana katika kile walichokiita kuwa ni 'mkutano mkuu wa dharura' na kutangaza kuupindua uongozi wa Rage na kukabidhi madaraka kwa 'kamati ya muda' iliyopendekezwa kuongozwa na Hanspope na mwanachama mwenzao, Rahma Al Kharoos 'Malkia wa Nyuki'.

Hata hivyo, mapinduzi hayo yaligonga mwamba baada ya kubainika kuwa yalikiuka katiba ya Simba huku pia yakipingwa na walioteuliwa kuongoza; Hanspope na 'Malkia wa Nyuki'.