come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KIINGILIO SIMBA NA YANGA CHATAJWA

MASHABIKI watakaotaka kwenda kushuhudia mpambano wa mahasimu wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam watalazimika kulipa Sh. 5,000, hicho kikiwa kiingilio cha chini zaidi katika sehemu ya viti vya Rangi ya Bluu. 


Aidha, katika mchezo huo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, utakaoanza saa 10:00 jioni, viingilio vingine ‘nafuu kidogo’ vitakuwa ni Sh 7,000 kwa viti ya Rangi ya Kijani na Sh. 10,000 kwa viti vya Rangi ya Chungwa.
Upande wa ‘wakubwa’, viingilio vitakuwa ni Sh. 15,000 kwa VIP C, Sh. 20,000 kwa VIP B na Sh. 30,000 kwa VIP A.

Ofisa Haabri wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema kwamba viingilio hivyo ni sawa na viingilio vya mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo baina ya miamba hao, Oktoba 3, mwaka jana. 

Wambura alisema tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo, yaani Ijumaa wiki hii katika vituo mbalimbali vitakavyotajwa.
Tayari miamba hiyo ya soka nchini iko mafichoni kwa maandalizi ya mpambano huo.

Yanga wameweka kambi yao kisiwani Pemba katika hoteli ya Samail mkabala na benki ya PBZ, wakifanya mazoezi Uwanja wa Gombani wakati Simba wameweka kambi maeneo ya Mbweni JKT Zanzibar wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung.

Wakati Yanga walitua Pemba Ijumaa jioni, mahasimu wao wa jadi, Simba SC waliwasili Zanzibar Jumapili jioni na mara moja kuanza kujifua kwa ajili mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu.