BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limewahimiza wadau kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi za uongozi wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro, Oktoba 26.
Awali, uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika Julai 7 jijini Mwanza, lakini kutokana na idadi ndogo ya wagombea waliojitokeza na kutotimia kwa akidi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa BFT, uliahirishwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BMT, Henry Lihaya, alisema wanaendelea kutoa fomu hadi siku nne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
“Nawaomba wadau waje kwa wingi kuchukua fomu, maana tunaendelea kuzitoa kwa kuwa tulikubaliana wagombea waliochukua katika mchakato wa mara ya kwanza wataendelea kuwania nafasi zao lakini ambao wanahitaji na hawajachukua waje milango iko wazi,” alisema Lihaya.
Alisema mchakato wa uchaguzi huo umeanza upya, ambapo fomu zinazotolewa ni kwa nafasi ya Rais, Makamu, Katibu Mkuu, Mweka Hazina na wajumbe tisa wa kamati ya utendaji.
Gharama za fomu hizo kwa nafasi ya Rais ni sh 150,000 huku Makamu, Katibu Mkuu na Mweka Hazina ni sh 100,000 na sh 50,000 kwa wajumbe.