Kufuatia ushindi mnono wa magoli 5-1 wa timu yake juzi dhidi ya Ashanti United ya jijini Dar es Salaam, kocha wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, Ernie Brandts, amesema kuwa kikosi chake hakikubahatisha, huku kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni akimuangushia zigo la lawama kipa mpya Abel Dhaira katika sare yao ya 2-2 dhidi ya Rhino.
Brandts alisema kuwa kasi hiyo ya ushindi itaendelea lakini alisisitiza kuongezeka kwa majeruhi katika kikosi chake ni hali inayomvurugia mipango yake kwa kumlazimisha kufanya mabadiliko ya lazima.
Mholanzi huyo alisema kwamba walifanya maandalizi mazuri kabla ya msimu na matokeo hayo hayakumshangaza kutokana na uwezo wa wachezaji wake alivyowaandaa.
Alisema kwamba anaamini timu yake itaendelea kupata matokeo mazuri kufuatia uzoefu walionao wachezaji wake ukilinganisha na wachezaji wa timu pinzani.
Alisema kwamba ataendelea kumpumzisha beki majeruhi Kelvin Yondani ambapo hafikikirii kumpanga keshokutwa Jumatano katika mechi ya raundi ya pili dhidi ya mabingwa wa mwaka 1988, Coastal Union, kutoka Tanga.
Wakati huo huo, Coastal ilitarajiwa kuwasili jijini jana usiku ikitokea Arusha tayari kuikabili Yanga. Coastal Union nayo ilianza vyema ligi kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya JKT Oljoro.
Kocha Kibadeni alisema kipa wao Mganda Dhaira na Shirikisho la Soka (TFF) ndiyo waliochangia timu yake kufanya vibaya katika mechi yao ya ufunguzi kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi juzi.
Akizungumza mjini hapa jana asubuhi, Kibadeni alisema Dhaira hakucheza vizuri na alikuwa kikwazo katika mechi ya hiyo iliyoshuhudiwa na watu 12,981 waliokata tiketi halali.