Golikipa Mtanzania Ivo Mapunda (Pichani) amesema Gor Mahia itakosa sana huduma za rama Salim.
Salim aliondoka nchini mnamo Jumapili na kuelekea Qatar, ambako
anatarajiwa kujiunga na klabu ya daraja la pili Al Marhiya. Anaondoka
Gor na kuiacha katikati ya safari na baada ya kuchangia sana kuifikisha
ilipo sasa, na itamkosa sana.
Mapunda aliongezea yakuwa Gor kama timu itakuwa dhaifu kiasi bila
yeye. Hata hivyo, anaamini kwamba bado watashinda Ligi Kuu ya Kenya
licha ya kuondoka kwake.
“Rama atakoswa sana. Amekuwa mchezaji muhimu sana kwa klabu hii.
Huwa kamwe hutaki kupoteza wachezaji muhimu kwenye timu kwani hilo huwa
na maana kwamba unadhoofika na hali ni hivyo kutokana na kuondoka kwake.
Ni mchezaji mzuri na utatatizika kumpata mwingine kama yeye. Namtakia
kila la heri na naomba afanikiwe.”
Licha ya Rama kuondoka, Mapunda bado anaamini kwamba Gor watashinda ligi ya KPL.
“Ligi bado inashindaniwa na mimi pamoja na wenzangu tunaamini kwamba tutashinda mwishowe,” akasema.
“Bado sisi ndio tunaopigiwa upatu na tunataka mambo yabaki hivyo.”