BAADA ya kutamba na kazi yake inayojulikana kwa jina la ‘Haipotei’, msanii wa muziki wa bongo fleva, Juma Kassim ‘ Sir Juma Nature’ (Pichani), anatarajiwa kuachia ngoma yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘Dogo’ hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Sir Nature alisema ngoma hiyo ameikamilisha na yupo katika hatua za mwisho za kuanza kuisambaza.
“Kazi hii imekamilika, kilichobaki ni kuisambaza katika vituo mbalimbali vya redio na kwa wale wanaotaka kuisikiliza, kuanzia kesho tembelea kwenye blogu ya tmkwanaumehalisi utaisikiliza kupitia humo na utatupia ‘comment’ zako kuhusu kazi hiyo,” alisema.
Aliwaomba samahani mashabiki wake kwa kukaa kimya muda mrefu na kuongeza kuwa, baada ya kuisambaza kazi hiyo katika vituo vya redio, ataanza maandalizi ya video muda wowote.
Licha ya kuandika kwenye ‘facebook’ kuwa, ngoma hiyo ingesikika wiki iliyopita, Nature alisema hakuweza kufanya hivyo kutokana na majukumu, hivyo siku yoyote kuanzia leo ataisambaza katika vituo mbalimbali vya redio.