Wagombea walioenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya usaili uliofanywa chini ya mwenyekiti, Hamidu Mbwezeleni ni pamoja na wagombea wawili wa nafasi ya urais, Richard Rukambura na Omary Nkwaruro.
Rukambura ameenguliwa kutokana na kitendo chake cha kufungua kesi mahakamani kwenye uchaguzi wa awali uliofutwa kupinga kuenguliwa kwake, wakati Nkwaruro yeye cheti chake kuwa na utata.
Kwa upande wa wajumbe walioenguliwa ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, Samwel Nyala na Eliud Mvela ambao walikuwa wanatetea viti vyao.
Akitangaza kuenguliwa kwa wagombea hao Ofisa Habari wa TFF, Bonifance Wambura alisema, Nyala ameenguliwa kwa vile hakujaza kikamilifu fomu ya maombi kwa kushindwa kusema malengo yanayomfanya ogombee, wakati Mvela ameenguliwa baada ya kuligeuka azimio lililopitishwa na kamati ya utendaji ya TFF aliposhiriki kutoa uamuzi wa mabadiliko ya katiba kufanyika kwa njia ya waraka na baadaye akayapinga hadharani hivyo suala lake litajadiliwa katika Kamati ya Maadili ya uchaguzi.
Wengine ni Abdallah Hussein (Kagera) ameondolewa kwa vile hakujaza fomu za uchaguzi na badala yake alituma fomu ya uchaguzi uliofutwa, wakati Stanlaus Nyongo (Shinyanga/Simiyu)ameondolewa kwa kigezo cha uzoefu huku Ayub Nyaulingo naye akiwa hana uzoefu wa miaka mitano.
Nazarius Uligeja pia ametupwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa madai ya kusababisha migogoro katika Chama cha Soka cha Rukwa na suala lake limepelekwa katika kamati ya maadili kujadiliwa, huku Cyprian Kuyava ameondolewa kwa kukosa uzoefu wa miaka mitano wakati Ayubu Nyenzi ameshindwa kuthibitisha uraia wake.
Kamwanga Rajabu (Njombe) ameenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na tuhuma zilizowahi kumkabili za kushiriki rushwa kwa waamuzi, huku Riziki Juma (Pwani/Moro) akiondolewa kwa kushindwa kusimamia kanuni za ligi akiwa mtendaji mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (Corefa) kipindi cha Ligi ya Mkoa na mmoja wa wadau wa soka akafungua kesi mahakamani. Kwa upande wa Kanda ya Dar es Salaam iliyokuwa ikiwaniwa na wajumbe watano, wameenguliwa watatu, Wilfred Kidau, Omary Abdukadir na Shafii Dauda.
Wambura alisema Kidau ameenguliwa baada ya kutumia nyaraka za kamati ya utendaji bila idhini wakati Dauda alitumia nyaraka za mawasiliano za Fifa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga na kuweka kwenye mtandao wa kijamii bila idhini huku Abdukadir akienguliwa kwa kushindwa kuheshimu maagizo ya TFF.