Hatimaye kiungo wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Kiggy Makasy (Pichani),
anatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu ijayo ya Septemba 9 mwaka huu
kwenda India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa goti la kulia imeelezwa
jana na uongozi wa klabu hiyo.
Awali kiungo huyo alitarajiwa kuondoka nchini Agosti 18 mwaka huu na
kwenda katika hospitali ya Saifee iliyoko India ili kufanyiwa upasuaji
huo.
Makassy aliumia wakati Simba ilipokuwa mkoani Dodoma ikicheza mechi ya
kirafiki dhidi ya CDA mwezi Aprili mwaka huu ambapo aliumia na kukaa nje
ya uwanja tangu wakati huo.
Makassy akiwa India atafanyiwa matibatu ya kuurejesha sawa sawa mguu
wake huo wa kulia uliochanika nyama ili aweze kurejea tena uwanjani.
Akizungumza jana jijini, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema
kuwa tayari maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na kilichobaki ni
kukutana na daktari wake na wanaamini baada ya matibabu atarejea
kuitumikia timu yake.
Simba pia iliwahi kumpeleka kiungo wake mwingine, Uhuru Suleiman, kupata matibabu India baada ya kuvunjika mguu mwaka juzi.