Zikiwa zimebaki siku tisa kabla ya Simba kuwavaa wapizani wake wa jadi Yanga, imefumua kikosi chake cha kwanza na kumpa onyo mshambualiji wake hatari, Betram Mombeki.
Simba inaivaa Yanga katika Ligi Kuu ya soka Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba 20, mwaka huu.
Uongozi wa Simba umethibitisha mbali na kumpa onyo Mombeki imewashusha kikosi cha pili wachezaji wake watano wakiwemo watatu wanaocheza kikosi cha kwanza tangu ligi ianze.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala aliwataja jana wachezaji waliosukumwa kikosi cha pili kwa madai ya kushuka kiwango ni Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Amri Kiemba, Haruna Chanongo, Edward Christopher na Henry Joseph.
Kiemba, Chanongo na Henry wamekuwa wakicheza kikosi cha kwanza ‘first eleven’ ya Simba ambayo imecheza mechi saba na kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 15.
Mtawala alidai kuwa hakuna mchezaji aliyesimamishwa kwa madai ya utovu wa nidhamu lakini Kocha Abdallah Kibaden amependekeza wachezaji hao warudi katika timu ya vijana.
Katika hatua nyingine wachezaji Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Miraji Adam wataukosa mchezo wa kesho dhidi ya Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Taifa kwa kuwa bado ni majeruhi.
Simba kwa sasa imejichimbia Bamba Beach ikijifua kwa ajili ya pambano la kesho na maandalizi ya mchezo wao na watani zao, Yanga ambao wapo Kagera kwa ajili ya kuikabiri Kagera Sugar