Siku moja baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kumwagiza Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kuitisha Mkutano Mkuu wa dharura wa klabu ndani ya siku 14 kuanzia juzi, Mbunge huyo wa Tabora Mjini amepuuza agizo hilo huku akikwea pipa na kwenda Uingereza.
Juzi Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema wameamua kutoa agizo hilo baada ya kubaini kuna mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha Rage, na nyingine kutoka kwa mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Simba zilizopo mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam, Rage alisema 'maagizo ya uongozi mpya wa TFF hayatekelezeki'.
Alisema TFF ilipaswa kutoa adhabu kwa 'wanamapinduzi' waliokutana Jumatatu jijini Dar es Salaam na kumsimamisha kinyume cha Katiba ya Simba Ibara za 22 na 28 (Muundo wa Kamati ya Utendaji ya Simba na mamlaka ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura) na Katiba ya TFF Ibara za 31 na 73.
Alisema Kamati ya Utendaji ya TFF ikiendelea kumtaka aitishe mkutano huo, atachukua maamuzi magumu ya kuachia ngazi ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.
"Nilipata barua jana (juzi) kutoka TFF ikinitambua mimi (Rage) kama mwenyekiti halali wa Klabu ya Simba, lakini nimesikitishwa na maagizo ya TFF mpya kunitaka niitishe Mkutano Mkuu wa dharura wa wanachama wa Simba. Maagizo haya ni kinyume na Katiba ya Simba na hata ya TFF," alisema Rage na kusisitiza:
"Hakuna kifungu hata kimoja ndani ya Katiba ya TFF kinachoeleza kuhusu maagizo waliyonipa. Kibaya zaidi wamekwenda mbali zaidi kwa kunipa siku 14 na kunichagulia ajenda, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Simba.
"Ibara ya 22 ya Katiba ya Simba inayotamka wazi kwamba mwenyekiti wa klabu anaweza kuitisha Mkutano Mkuu wa dharura kwa kushirikiana na kamati ya utendaji kama anaona inafaa kufanya hivyo.
"Sasa nawaambia TFF kwamba, kama mwenyekiti wa Simba siitishi mkutano huo, na nimeshawaandikia barua leo (jana) kuwafahamisha kuhusu hilo. Wakiendelea kung'ang'ania, nitajiuzulu kwa sababu nalindwa na katiba. Mimi ni Mbunge na nimeitoa mbali sana Simba. Nimechoka kuchafuliwa, nimenyanyaswa na nimedhalilishwa sana," alifafanua zaidi Rage.
Katika kuthibitisha kwamba anajua anachokisema, Mbunge huyo wa Tabora Mjini (CCM), jana alikuwa na 'furushi' kubwa lililosheheni nyaraka mbalimbali zikiwamo Katiba za Simba, TFF, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na kanuni za maadili za mashirikisho hayo.
Rage pia alikuwa na nyaraka muhimu za makubaliano yao na Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia waliyomuuza mshambuliaji wao wa zamani, Mganda Emmanuel Okwi Julai mwaka jana na kueleza kwa kina sababu zilizokwamisha kulipwa kwa fedha ya uhamisho wa mchezaji huyo.
KIKAO CHA HARUSI
Aidha, Rage alisema Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jijini Jumatatu bila uwapo wake, kilikuwa sawa na kikao cha mipango ya sherehe za harusi kwani hakikuzingatia matakwa ya Ibara ya 22 ya Katiba ya Simba ambayo inatamka wazi mwenyekiti ndiye mwenye mamalaka ya kuitisha mkutano wa kamati ya utendaji.
"Kikao cha Itang'are (Joseph) na wenzake kilikuwa cha harusi. Nilitegemea taarifa ya kwanza ya TFF mpya ingelikuwa kulaani 'mapinduzi' yaliyofanywa dhidi yangu kwa sababu ibara ya 73 ya Katiba ya TFF na kanuni za maadili za shirikisho zinatamka wazi, watu wanaotaka kufanya mapinduzi ya uongozi wa TFF na wanachama wake kufungiwa kujishirikisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyozidi 10," alisema Rage.
MALINZI ALONGA
Malinzi alisema kwa simu jana atatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo baada ya kupata taarifa rasmi kutoka kwa Rage.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura aliliambia gazeti hili jana kuwa bado hawajapata barua ya Mwenyekiti huyo wa Simba kuhusu kukataa kwake kutekeleza maagizo ya TFF.
Wakati huo huo, Rage jana alitangaza kumteua Katibu Mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT sasa TFF), Michael Wambura kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba huku akieleza kwamba ameongea na mwanachama wao tajiri, Rahma Al Kharusi 'Malkia wa Nyuki' ambaye amekubali kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, hivyo jina lake atalipeleka kwenye mkutano mkuu ujao ili lijadiliwe na wanachama wa klabu hiyo.
MAREKEBISHO YA KATIBA
Aidha, Rage alisema leo anaondoka nchini kwenda Uingereza akiwa na wajumbe wenzake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma