come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

ZITO KABWE ADAI KULA SAHANI MOJA NA MBOWE, SLAA.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amesema kuwa hana mpango wa kujiondoa Chadema na kusisitiza kwamba atakuwa mtu wa mwisho kujitoa ndani ya chama hicho kwa hiari yake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana katika mkutano aliouandaa kwa pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alisema kwamba amekuwa mwanachama wa Chadema tangu akiwa na umri wa miaka 16 hivyo haiyumkiniki akikimbia chama hicho.

Zitto na Dk Kitila walivuliwa nyadhifa zao wiki iliyopita wakihutumiwa kukihujumu chama hicho.

“Kuna watu ambao walitegemea kuwa leo hii ningejibu mapigo, ‘ningezodoa,’ watu wengine kwa majina kama ilivyo kawaida kwa siasa za Tanzania. Natambua pia kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro kwa vyama hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza kinachoitwa ‘maamuzi magumu’,” alisema na kuongeza:

“Natambua kuwa wapo ambao wangependa kutumia nafasi zao kudhoofisha mapambano ya siasa za demokrasia nchini mwetu, napenda wanachama wa Chadema na wapenda demokrasia wote nchini watambue kuwa, mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwa hiari yangu.”


“Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.”

Alisema kuwa atafuata taratibu zote za ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hilo.

“Mimi sitoki, wanaotaka nitoke, wanitoe wao,” alisema Zitto.

Zitto alisema Chadema ndicho chama kilichomlea na kumfikisha hapo alipo sasa, hivyo hata siku moja hatokuwa chanzo cha kuvunjika kwa chama hicho.

“Ningependa hata mtoto wangu akikua, awe pia mwanachama wa chama hiki, nimejiunga na chama hiki nikiwa na umri wa miaka 16 mpaka sasa nina miaka 37, nimetumia muda mrefu zaidi Chadema kuliko kipindi chote cha maisha yangu, Chadema ni kama maisha yangu, kukivunja chama hiki ni sawa na kujivunja mimi mwenyewe, kitu ambacho siwezi,” alisema Zitto.