Kocha wa Yanga, Ernie Brandts (pichani chini) amesema kikosi chake kitafanya vizuri katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani licha ya kupangwa kukutana na mabingwa watetezi, Al Ahly katika raundi ya kwanza.
Yanga, ambao wako kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mchezo wa 'Nani Mtani Jembe' dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, wataanza mashindano hayo kwa kucheza nyumbani dhidi ya 'vibonde' Komorozine ya Comoro katika hatua ya awali na wakifuzu watavaana na Al Ahly ya Misri.
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Grand Malt Zanzibar, KMKM wataanzia ugenini dhidi ya Dedebit ya Ethiopia wakati wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC wataanzia nyumbani dhidi ya Ferroviario Da Beira ya Msumbiji.
Wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Chuoni wataanzia nyumbani pia dhidi ya How Mine ya Zimbabwe.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Jumatatu, mechi za kwanza zitachezwa kati ya Februari 7-9, wakati marudiano yatakuwa kati ya Februari 14-16, 2014.
Akizungumza mara tu baada ya kumalizika kwa mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana asubuhi, Brandts (57), alisema kikosi chake kiko vizuri na kitaishangaza dunia kwa kuwapiga Al Ahly.
"Kwa kutambua tutashiriki mashindano ya kimataifa mwakani, tumeanza maandalizi mapema, mipango yetu iko safi na tumefanya usajili mzuri. Sina wasiwasi wowote na kikosi changu licha ya kupangwa na mabingwa Al Ahly. Yanga ina wachezaji wazuri wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa. Tutawafunga Al Ahly na kuwashangaza wengi," alisema Brandts.
KWENDA COMORO JANUARI
Aidha, beki huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Uholanzi alisema atakwenda nchini Comoro kuwasoma wapinzani wao katika raundi ya kwanza, timu ya Komorozine.
"Siwajui Komorozine, baada ya ratiba kutoka juzi (Jumatatu), jana (juzi) nilikutana na uongozi kujadili namna ya kuifuatilia timu hiyo ili tujue mbinu zao. Wiki tatu kabla ya kucheza nao nitakwenda Comoro kuangalia mechi zao. Tutatafuta pia video za mechi zao," alisema Brandts.
Droo iliyochezeshwa Jumatatu mjini Marrakech, Morocco ilionyesha kuwa klabu 52 zitamenyana katika raundi ya awali ya michuano ya 18 ya Ligi ya Mabingwa mwakani kusaka nafasi za kuungana na mabingwa watetezi, Al Ahly, Coton Sport ya Cameroon, TP Mazembe ya DRC, Hilal ya Sudan, CS Sfaxien na Esperance Sportive za Tunisia katika raundi ya kwanza.