Pamoja na makocha wengi kujitokeza kuwania nafasi ya kuinoa Yanga, uongozi wa klabu hiyo umeelekeza nguvu zao Uingereza kwa ajili ya kurithi mikoba ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Yanga, mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji na mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya kimataifa, Seif Ahmed ‘Magari’ tayari wapo mjini London kwa ajili ya kusaka kocha mpya wa timu hiyo Yanga.
Pamoja na taarifa kuwa Manji yupo huko kwa shughuli zake, chanzo chetu kimesema kuwa mwenyekiti huyo aliifanya kazi hiyo na baadaye Seif ‘Magari’ kwenda kuongeza nguvu.
Chanzo chetu kilisema kuwa kazi hiyo inaenda vizuri kiasi cha wajumbe wa kamati ya kusaka kocha mkuu wa Yanga waliopo Tanzania kupunguza kasi kwa kile kilichosemwa kuwa ‘tayari’ kuna mafanikio ya kupata kocha mpya.
Taarifa hizo zimesema kuwa kesho, uongozi Yanga utakutana kabla ya kukutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kuweka wazi masuala mbalimbali ikiwa pamoja na suala la kocha mkuu.
Masuala mengine ambayo yatajadiliwa ni hatima ya kocha msaidizi, Fred Minziro ambaye inasadikiwa nafasi yake itachukuliwa na kocha mkuu, Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa.
Pia mkutano huyo utatoa hatma ya ushiriki wa Yanga katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi na safari ya Hispania kwa ajili ya kambi.
Taarifa hizo zimesema kuwa mpaka sasa hakuna anayejua kama Yanga itashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuwa timu hiyo ina mpango wa kuweka kambi nchini Hispania au Uturuki.
Kama Yanga watashiriki Kombe la Mapinduzi litalomalizika Januari 13, watakuwa na siku 10 za kujiandaa nje ya nchi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyopangwa kuanza Januari 25.