KOCHA Mkuu wa Simba SC, Zdravko Logarusic jana alijikuta anamzaba kibao Msaidizi wake, Suleiman Matola ‘Veron’ wakati anamuelekeza mambo kwenye benchi, kabla ya kuanza kwa mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi, baina ya timu yake na KMKM Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Zdravko, raia wa Croatia aliinuka na Matola kwenda kuungana na wachezaji 11 waliowateua kuanza mechi ya jana, Yaw Berko, William Lucian ‘Gallas’, Omar Salum, Gilbert Kaze, Donald Musoti, Abdulhalim Humud, Uhuru Suleiman, Amri Kiemba, Betram Mombeki, Ali Badru na Edward Chistopher kupiga nao picha na baada ya hapo wakarudi kwenye benchi.
Walipofika kwenye benchi Zdravko akaanzisha mazungumzo yaliyomhusisha pia Meneja wa timu, Nico Nyagawa ambayo yaliambatana na mifano, vicheko na furaha tele.
Ikatokea Zdravko anatoa mfano wa kumpiga mtu kibao na akampelekea cha ukweli Matola usoni, lakini chepesi.
Baada ya kushitukia kamera ya waandishi ilikuwa inafanya mambo wakati wakiendelea na zoezi lao, wakaacha mara moja na kuanza kuangalia mechi.
Katika mchezo huo, Simba SC ilishinda bao 1-0 na kufuzu Robo Fainali kama mshindi wa pili wa Kundi B, kwa pointi zake saba, mabao mawili ya kufunga na haijafungwa, ikiwa nyuma ya KCC ya Uganda yenye pointi saba pia, mabao sita ya kufunga na mawili ya kufungwa.
Bao la Simba SC lilifungwa na kiungo mtaalamu, Amri Ramadhani Kiemba kwa kichwa, akiunganisha krosi maridadi ya Ali Badru Ali dakika ya tano.
KMKM sasa inasubiri mustakabali wake wa kusonga mbele katika nafasi mbili maalum kwa makundi yote, kuungana na timu sita zitakazofozu moja kwa moja kutoka makundi hayo.