come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: NI DEO MUNISHI TU ANAPASWA KUIOKOA YANGA APRIL 19

Na Fikiri Salum

HALI si shwari katika kikosi cha Yanga kwa sasa, mambo yanakwenda kinyume na matarajio yake, mikakati ya Yanga ilikuwa kusonga mbele katika michuano ya kimataifa, lakini ikajikuta inasukumwa nje na kuanza upya.

Tayari Yanga imetolewa na mabingwa wa zamani wa ligi wa Afrika, Al Ahly ya Misri ambao nao wametupwa nje na Al Ahly Benghazi ya Libya juma lililopita, Yanga imerejea katika ligi kuu ya bara ili kutetea ubingwa wake ama kusaka nafasi ya pili ili irejee tena katika michuano ya kimataifa.

Hata hivyo mambo yanaonekana kuwa mabaya katika kikosi hicho cha Yanga, mbali ya kuonekana kushindwa kutetea taji lake kiuhakika na sasa inaombea mpinzani wake mkuu katika mbio hizo za ubingwa Azam fc iteleze angalau michezo miwili ili watetee taji lao.

Hiyo inawezekana ni kazi ngumu sana isitoshe Azam imebakiza mechi tatu na hadi sasa haijapoteza hata mchezo mmoja, kwa wachambuzi wa soka kama sisi tunajua nini kimepelekea Yanga kupotea msimu huu.


Yanga inatafuta nafasi ya pili tu kwani ubingwa uko rehani, katika vita hiyo ya nafasi ya pili Yanga ina ushindani mkubwa na vijana wa Mbeya City ambao wanaonesha kufufua matumaini yao ya kushika nafasi hiyo badala ya tatu waliyokuwa wakiipigania.

Kuumia kwa mlinda lango nambari moja wa Yanga Deogratus Munishi 'Dida' kumepelekea kikosi hicho kupoteza mwelekeo katika mechi zake zilizosalia, huenda Yanga ikakamata nafasi ya tatu ama ya pili kama itazicheza vema karata zake ilizobakiwa nazo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya bara walijikuta wakipoteza mchezo muhimu dhidi ya vibonde JKT Mgambo ya Tanga, katika mchezo huo Yanga ililala mabao 2-1 hivyo kuuweka rehani ubingwa wake kwa Azam fc.

Kufungwa kwa Yanga kulisababishwa na uzembe wa makusudi wa baadhi ya wachezaji huku kipa Juma Kaseja akionekana dhahiri kurudiarudia makosa, ikumbukwe mwaka jana Yanga ilifungwa na hasimu wake Simba katika mchezo wa kirafiki uliofahamika kwa jina la Nani mtani jembe.

Yanga ililala mabao 3-1, magoli mawili yalichangiwa na Kaseja, Kaseja alishindwa kuupiga mbele mpira aliorudishiwa na beki wake ambapo alianza kuzubaa nao kisha kutaka kumlamba chenga mshambuliaji wa Simba ambaye aliunasa na kuuweka kimiani.

Mashabiki wa Yanga walichukizwa sana na goli hilo, walidai ni uzembe wa kipa, uongozi wa Yanga ulionyesha kumlinda Kaseja na kuanza kulitimua benchi lake la ufundi ambapo Mholanzi Ernie Brandts kocha ambaye aliahidi kuifikisha Yanga robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika na msaidizi wake Fred Minziro walitimuliwa.

Kutimuliwa kwa makocha hao kulienda sambamba na kutimuliwa kwa kocha wa makipa Razzack Ssiwa na daktari wa timu Nassoro Matuzya.

Uzembe wa Kaseja uliigharimu tena Yanga na kuondoa ndoto yake ya kutetea taji la ubingwa wa Tanzania bara msimu wa 2013/14, Kaseja alirudia makosa yale yale ambapo alirudishiwa mpira na beki wake Kelvin Yondani badala ya kuupiga mbele yeye alibaki kupasiana na Yondani na kupelekea mfungaji wa goli la Mgambo kuukaribia na kuupachika wavuni.

Ni goli lililowaumiza Wanayanga wote, ila yote hayo yametokea baada ya mlinda lango tegemeo katika kikosi hicho Deogratus Munishi 'Dida' kuwa nje ya uwanja baada ya kupata majeraha wakati akiisaidia Yanga katika michuano ya ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Dida aliumia katika mchezo huo huku akiwa shujaa wa Yanga, katika mchezo huo Yanga ilitolewa na mabingwa hao wa zamani wa Afrika kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kufungana mabao 1-1 katika mechi zote mbili za nyumbani na ugenini.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam Yanga ilishinda bao 1-0 hivyo katika mchezo huo wa marudiano uliofanyika jijini Alexandria Misri Al Ahly nao walishinda 1-0 na kufanya matokeo yasomeke 1-1.

Mikwaju ya penalti ndio iliyoiua Yanga ambapo shuti la mshambuliaji wake Said Bahanuzi lilipaa nje ya lango na kufanya Yanga ishindwe kuibuka na ushindi hivyo kuchanganyikiwa kisaikolojia na penalti iliyobakia ilikoswa pia na Mbuyu Twite.

Yanga sasa imesaliwa na mechi nne mkononi, ili iweze kukamata nafasi ya pili kama si ubingwa basi inahitaji ishinde mechi zote hizo, lakini kama itaendelea kumtumia Kaseja katika michezo iliyobakia basi itaambulia patupu.

Dida ndiye kipa pekee katika kikosi hicho anayewe kucheza kwa kujitoa kwa moyo wote, kiwango cha Dida kimeonekana kuimarika tangia lipoanza kuidakia Yanga baada ya kipa Ally Mustapha 'Barthez' kuigharimu Yanga katika mchezo wake dhidi ya Simba.

Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 3-0 hadi mapumziko, kipindi cha pili Simba walisawazisha mabao yote matatu na kuwa 3-3 huku magoli ya Simba yalifungwa kutokana na uzembe wa Barthez.

Dida anasalia kama kipa tegemeo katika kikosi cha Yanga msimu huu na anastahili kuongezewa mkataba mwingine mara tu huu wa sasa utakapomalizika, amecheza mechi kumi za ushindani ameruhusu goli nne tu langoni mwake.

Tofauti na Juma Kaseja au Ivo Mapunda wa Simba, Kaseja amecheza mechi nane za ushindani akiwa na Yanga ameruhusu mabao sita, bila shaka tumwombee afya njema Dida ili arejee uwanjani katika mechi zinazofuatia ikiwemo ile na mtani wa jadi Simba ambayo itachezwa April 19 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa.

Matarajio ya Wanayanga ni kuona kikosi chao kinafanikiwa tena kushiriki michuano ya kimataifa mwakani iwe ligi ya mabingwa barani Afrika au kombe la shirikisho, kuteleza si kuanguka.